Habari

Profesa Sunguya: Maonesho kazi za bunifu, tafiti za kisayansi kusaidia upatikanaji wa wanasayansi

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) Profesa Bruno Sunguya amesema uwepo wa maonesho ya kazi za bunifu za kisayansi zinazofanywa na wanafunzi zitasaidia kupatikana kwa wanasayansi wa kutosha nchni.

Sunguya ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa wanafunzi wa sekondari waliofanya tafiti na bunifu za kisayansi zilizoandaliwa na Shirikisho la Wasayansi Chipukizi Tanzania (YST).

Profesa Sunguya ambaye alimwakilisha Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda amesema uwepo wa maonesho hayo ya bunifu na tafiti za kisayansi pia zinaibua hamasa kwa wanafunzi na kuwafanya kuyapenda masomo hayo.

“YST walikusanya zaidi ya tafiti na gunduzi za kisayansi 1500 za wanafunzi lakini kati ya hizo 900 zilichujwa na kupatikana washindi katika mashindano hayo muhimu ambayo yanahamasisha ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia,” amesema Profesa Sunguya

Aidha Profesa Sunguya ameishukuru Taasisi ya Karimjee kwa kuwa mdau mkubwa na muhimu katika mashindano hayo akishirikiana na taassi zingine kwa lengo la kuinua sayansi na kuhamsha hali ya ubunifu hapa nchini.

Hata hivyo amesema nchi yetu inahitaji wanasayansi wa kutosha na ili kuweza kufanikisha lengo hilo ni lazima kuwaelimisha wanafunzi na kuwasihi kupenda masomo ya sayansi wakiwa wadogo.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya YST, Profesa Yunus Mgaya amesema kupitia maonesho hayo ya bunifu na tafiti za kisayansi yanasaidia kupata wanasayansi wengi.

Amesema anawapongeza wanafunzi wote walioshiriki katika maonesho hayo kwani wameonesha wazi kuwa taifa litapata wanasayansi wengi katika siku zijazo.

Kwa upande wake Mwanzilishi mwenza wa shirikisho hilo, Dk Gozibert Kamugisha amesema maonesho hayo yanafanyika ili kutambua mchango mkubwa hasa wa ubunifu na utafiti unaofanywa na wanafunzi mbalimbali wa sekondari.

“Ni mwaka wa 13 sasa tunafanya maonesho haya ambayo yamekuwa yakisisitiza teknolojia, YST inaibua na kutengeneza wanasayansi wachanga hapa nchini,” amesema Kamugisha

Mwakilishi wa Taasisi ya Karimjee Foundation ambaye ni mdhamini mkuu wa maonesho hayo, Vinoo Somaiya amesema taassi hiyo itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wote watakaoshinda.

Amesema lengo la kufanya hayo ni kuendelea kuhamasisha wanafunzi kupenda kusoma masomo ya sayansi na teknolojia na hatimaye kuja kuwa wabunfu.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents