
Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kinachoendelea Israel ni “kibaya”, huku akitoa wito kwa pande zote mbili kupunguza vifo vya raia.
Akizungumza katika mkutano mjini Moscow, Putin – ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai ICC, kuhusu madai ya uhalifu wa kivita unaohusiana na Ukraine – pia aliishutumu Marekani kwa kuchochea hali ya wasiwasi.
“Sielewi kwa nini Marekani inaleta meli ya kivita [katika eneo hilo]”, alisema – akimaanisha Marekani kutuma msaada wa ziada wa kijeshi kwa Israel.
Na Putin pia alisema madai kwamba Iran inahusika katika shambulio la Hamas “hayana msingi” – ingawa inafaa kukumbuka kuwa Urusi na Iran zina uhusiano wa karibu, na Iran hata inachukuliwa kuwa mfadhili mkuu wa kijeshi wa Urusi.
Iran imeshangilia shambulio la Hamas dhidi ya Israel lakini kiongozi wake mkuu hapo jana alikanusha kuhusika.
Tehran imekuwa mmoja wa wafadhili wakuu wa Hamas kwa miaka mingi, ikitoa msaada wa kifedha na silaha.
Rais wa Poland amependekeza kuwa Putin anaweza kufaidika na mzozo wa Israel, akitumai huenda ukavuruga vita vya Ukraine – ingawa Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Grant Shapps alisema “hakuna nafasi” ya kupoteza mwelekeo katika vita.