HabariSiasa

Raila Odinga atangaza maandamano mara mbili kwa wiki

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametangaza kuwa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya sasa utafanya maandamano makubwa mara mbili kwa wiki.

Akihutubia wanahabari muda mfupi uliopita, Raila alitangaza kuwa watakuwa wakiingia mitaani kila Jumatatu na Alhamisi kila wiki hadi matakwa yao yatakaposhughuliiwa.

“Katika kukabiliana na matakwa ya umma, sasa tutafanya maandamano kila Alhamisi na Jumatatu kuanzia wiki ijayo,” Raila alitangaza.

Huku hayo yakijiri Rais William Ruto amesema kwamba hatakubali “kutoijali nchi” baada ya maandamano ya ghasia kukumba mji mkuu, Nairobi na mji wa Kisumu magharibi mwa Kenya.

Rais Ruto amemshutumu Bw Odinga kwa kujaribu kuanzisha mgogoro kwa mara ya pili, akisema alifanya vivyo hivyo baada ya uchaguzi wa 2017 na kumlazimisha Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta kufikia makubaliano ambayo yalimpa nafasi ya kuingia serikalini.

Siku ya Jumatatu, akizungumza katika kitongoji cha Kamukunji viungani mwa Nairobi,Raila alisema hatua hiyo ya maandamano haitaisha hadi Wakenya wapate kile ambacho ni chao kwa haki.

Aidha, alikemea nguvu iliyotumiwa na maafisa wa polisi Jumatatu, Machi 20, ambapo viongozi kadhaa wakuu wa mrengo wa upinzani na wafuasi wao walikamatwa.

Waziri Mkuu huyo wa zamani pia aliwaamuru wafuasi wake kususia bidhaa kadhaa ikiwa ni pamoja na chombo kimoja cha habari, benki moja ya kitaifa na kampuni moja ya simu.

Lakini Baraza la Habari Kenya, MCK, pamoja na Chama cha Wanahabari Kenya, KUJ, wamelaani hatua hiyo.

Odinga aliwataka wafuasi wake kususia gazeti la The Star akidai limekuwa likindeleza ajenda ya serikali ya Ruto ya ”kuwadhulumu Wakenya”.

Lakini MCK na KUJ wanasema hatua hiyo inatishia uhuru wa vyombo vya habari.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents