HabariSiasa

Raila Odinga atishia kuanzisha maandamano tena Kenya

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametishia kuanzisha tena maandamano dhidi ya serikali iwapo utawala wa Rais William Ruto utashindwa kushughulikia masuala aliyoibua wakati wa maandamano.

Bw Odinga mnamo Jumatatu alisitisha maandamano na kukubali kufanya mazungumzo na Rais Ruto.

Akizungumza Jumanne, alisema kauli ya Rais Ruto siku ya Jumapili, alipomtaka Waziri Mkuu huyo wa zamani kusitisha maandamano ya kupinga serikali nchini kote, haikugusia matakwa yaliyotolewa na upinzani.

Rais Ruto alitoa wito wa mazungumzo ya pande mbili bungeni kuhusu kuundwa upya kwa tume ya uchaguzi lakini hakugusia jinsi serikali yake inanuia kukabiliana na gharama ya juu ya maisha nchini.

Bw Odinga ametaka serikali ichukue hatua za haraka kupunguza gharama ya maisha na Rais Ruto kupanua mazungumzo yao zaidi ya bunge.

Alisema mchakato wa bunge hauwezi kushughulikia matatizo yao na kupendekeza kuundwa kwa timu sawa na Mkataba wa Kitaifa wa 2008, ambao ulisimamiwa na mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo Koffi Annan.

“Tunawahakikishia watu wetu na Wakenya kwamba macho yetu yameelekeza kwenye mpira, na tunasisitiza kwamba tutarejea kwa watu mapema kabisa kukiwa na ukosefu wa umakini kwa upande mwingine,” Bw Odinga alisema.

Mkuu huyo wa upinzani pia alidai kuwa kulikuwa na majaribio ya kuvuruga seva za uchaguzi, ambazo anataka zikaguliwe tena.

Akizungumza nchini Rwanda siku ya Jumanne, Rais Ruto alifutilia mbali uwezekano wa kuwepo kwa makubaliano yoyote yatakayoshirikisha upinzani ndani ya serikali yake.

Bw Odinga alikuwa ameitisha maandamano mara mbili kwa wiki baada ya kukataa matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana na kukosoa jinsi serikali inavyoshughulikia mzozo wa gharama ya maisha.

Kulikuwa na mapigano kadhaa kati ya polisi na waandamanaji vijana.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents