HabariSiasa

Raila Odinga atoa tamko tena, hatutaki maridhiano

Kiongozi wa Muungano wa Azimio Raila Odinga ameahidi maandamano makubwa zaidi dhidi ya serikali kuwahi kutokea, akiwaomba wafuasi wake kujitokeza kwa wingi Jumatatu- japo kwa amani.
Raila, ambaye alihutubia wanahabari siku ya Alhamisi, alipuuzilia mbali mapendekezo ya mapatano kati yake na Rais Ruto na kudai kuwa muungano wa Azimio hautaafikiana na ‘serikali haramu’.

“Tunatoa wito kwa Wakenya wote wazalendo kujitokeza kwa wingi kwa mama wa maandamano yote jijini Nairobi mnamo Jumatatu (Machi 27), na kufanya hivyo kwa amani,” Raila alisema.

Kulingana na Raila, madai ya serikali ya Kenya Kwanza kwamba Azimio anashinikiza kupeana mkono hayana msingi na ni uongo.

“Kenya Kwanza imeendelea kudai kuwa tunachotafuta ni kupeana mkono tu. Tunakanusha vikali uvumi huu usio na msingi. Hili ni dharau kwa akili ya Wakenya. Hatutashiriki kupeana mkono na utawala haramu,” aliongoza.

Kanusho la Bw Odinga linakuja kufuatia Maaskofu wa Kanisa Katoliki kumshauri kutafuta njia mbadala za kueleza malalamishi yake.

Maaskofu hao, kwenye kikao na wanahabari Jumatano, walitoa wito kwa Rais Ruto na Raila kuzingatia mazungumzo kama njia ya kumaliza mkwamo uliopo.

“Jibu letu kwa makasisi kuhusu maandamano yetu linapatikana katika Biblia na tunatafuta ukweli kwenye seva ya uchaguzi, kupunguza gharama ya maisha, kufuta uteuzi wa CAS 50 na kurejesha ‘Cherera Four’,” Raila alisema.

Wakati uo huo, mkuu wa upinzani alikashifu agizo la mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Ezra Chiloba kuhusu vyombo vya habari vinavyoangazia maandamano dhidi ya serikali, akisema ni njama ya kuingilia uhuru wa wanahabari.

Aliitaka Mamlaka hiyo kupitia upya ‘agizo hilo lililopitwa na wakati’.

Odinga aliandamwa na vinara kadhaa wa Azimio akiwemo Martha Karua, Kalonzo Musyoka, Eugine Wamalwa na Junnet Mohamed.

Alisisitiza kuwa maandamano ya kila wiki mbili yataendelea hadi serikali itakapozingatia matakwa yao.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents