HabariSiasa

Rais amsamehe mchugaji aliyemuita Pepo akidai anakamata raia wake kama Punda

Mchungaji na waziri wa zamani wa sheria wa Equatorial Guinea, ambaye aliwekwa kizuizini miaka miwili iliyopita kwa kumwita rais “pepo”, ameachiwa huru.

Rubén Maye Nsue Mangue aliachiwa huru baada ya kusamehewa na Rais Teodoro Obiang Nguema.

Bw Obiang, 82, ndiye mtawala aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika, baada ya kuchukua mamlaka katika mapinduzi mwaka wa 1979.

Bw Mangue alikamatwa kwa kumkosoa katika kanda ya sauti iliyosambazwa sana mitandaoni mwaka wa 2022, akimuita “pepo… kwa kuwashikilia watu wake kama wafungwa”.

Alikataa kuomba msamaha kwa mkuu wa nchi, hatua ambayo ilimfanya kufunguliwa mashtaka kwa kuchochea ghasia za umma huku wizara ya haki pia ikamfungia kuhubiri.

Bw Obiang ametajwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kuwa mmoja wa viongozi wakiimla barani Afrika.

Alishinda muhula wa sita katika uchaguzi wa 2022, kwa takribani 95% ya kura.

Upinzani katika taifa hilo lenye utajiri wa mafuta hauna nafasi na ukosefu wa vyombo vya habari huru umezidi kudidimiza matumaini.

Siku ya Jumatatu, Bw Mangue aliambia shirika la habari la AFP kwamba hakuwahi kuzungumza na wakili wakati wote alipokuwa kizuizini, na kwamba hakuwa amefikishwa mahakamani.

“Nilikuwa katika kizuizi cha kutengwa,” alinukuliwa akisema.

Amri iliyotolewa Ijumaa ilimpa Bw Mangue na wengine 19 msamaha.

Bwana Mangue ni mchungaji wa Kipentekoste aliyetawazwa rasmi, kuhudumu katika Kanisa la Prophetic Ministry of the Shadow of Christ.

Alikuwa waziri wa sheria kuanzia 1998 hadi 2004 alipofutwa kazi kufuatia tofauti kati yake na rais.

Mnamo 2007, Mangue aliteuliwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Equatorial Guinea katika Umoja wa Afrika na balozi wa Marekani mnamo 2013.

Mwaka uliofuata, alishukiwa kumpiga msichana katika makazi yake ya Marekani, lakini hakukamatwa kwa sababu alikuwa na kinga ya kidiplomasia.

Bw Mangue hakutoa kauli yoyote kuhusiana na tuhuma hizo wakati huo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents