Habari

Rais Mwinyi atoa maagizo Tantrade kufanya utafiti, ataka kodi, tozo ziondolewe bidhaa za mkakati

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameitaka Mamlaka ya Biashara Tanzania (TanTrade) kufanya utafiti wa uhakika kubaini masoko mapya ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, na kutoa taarifa hizo kwa Wafanyabiashara ili waweze kuyafikia masoko hayo kwa urahisia.

Ameyasema hayo leo Julai 13, 2024 wakati akifunga maonesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara Dar es salaam (DTIF) na kuongeza kuwa Serikali hizo zina nia thabit ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

“Wigo wa masoko umepanuka na kutoa fursa ya kufanya biashara na nchi za jumuiya nane za Afrika,Tantrade fanyeni tafiti za uhakika wa masoko mapya ya bidhaa na leteni taarifa kwa wafanyabiashara wazichangamkie,”amesema.

Hata hivyo amezitaka Wizara na Taasisi zinazohusika na biashara na uwekezaji katika Serikali ya Zanzibar na Jamhuri Muungano wa Tanzania, kuondoa urasimu na tozo kwenye maeneo ya kimkakati pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara.

Amesema maonesho hayo ya kimataifa yenye kaulimbiu ya “Tanzania ni mahali sahihi pa biashara na uwekezaji” yanakwenda sambamba na azma ya serikali ya kufungua nchi katika masoko pamoja na kuvutia uwekezaji.

“Nitoe wito kwa taasisi zetu zinazosimamia biashara na uwekezaji kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kuondoa urasimu na kuwezesha biashara zaidi, tunalenga kurahisisha biashara katika maeneo ya kimkakati ili kuchangia pato la Taifa na pato la mwananchi mmoja mmoja” amesema Dkt. Mwinyi.

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo amesema maonesho hayo yametoa fursa ya elimu kwa Wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi ambapo pia yaketoa fursa ya masoko.

Amesema Tanzania ni sehemu salama ya kufanya biashara na uwekezaji ambapo amewaalika Wafanyabiashara kufanya uwekezaji nchini.

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaban amewakaribisha Wafanyabiashara katika maonesho ya utalii na uwekezaji yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 25 na 26 mjini Zanzibar.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Hamis amesema jumla ya taasisi na watu binafsi 3,886 wameshiriki katika maonesho hayo ambayo kwa mwaka huu yamekuwa na mafanikio makubwa ikiwepo kufungua masoko na mahusiano kwa Wafanyabiashara wa nchi mbalimbali.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents