Rais Samia ataja mambo sita aliyoacha Hayati Msuya kama funzo kwa viongozi wa sasa

Rais Samia Suluhu Hassan ametaja mambo sita ambayo Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania hayati mzee Cleopa Msuya ameacha kama funzo kwa viongozi wa sasa, huku akieleza kuwa mambo hayo aliyoyafanya mzee huyo yataishi katika mioyo, akili na maisha ya viongozi na Watanzania.
Rais Samia alitaja mambo hayo jana wakati akiwasilisha salamu za rambirambi katika Ibada ya kumuombea hayati mzee Msuya iliyofanyika kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Kristo Mchungaji Mwema, Usharika wa Usangi Kivindu, Dayosisi ya Mwanga, Jimbo la Kaskazini mkoani Kilimanjaro.
Alisema miongoni mwa mambo hayo, Mzee Msuya alipenda maendeleo na kutoacha kuyasimamia yale aliyoyaamini pasipo kuyumbishwa na kitu chochote.
“Alifanya kila namna kusimamia kile alichokiamini na kufanyakazi kwa uzalendo na uadilifu mkubwa pia mzee Msuya aliamini katika usimamizi wa karibu wa raisilimali za Taifa ili zilete tija kwa wananchi.l,” Alisema Rais Samia
Alisema mzee Msuya pia aliamini kuwa ujuzi na utaalamu una nafasi kubwa katika kuleta maendeleo pia aliheshimu maoni na ushauri wa kitaalamu kutumia wataalamu kumuongoza na kumsimamia katika kuamua mambo mazito na kwamba hakuwa muoga wa mabadiliko.
“Mzee Msuya aliamini mabadiliko no hatua katika maendeleo na alifanyakazi kwa umakini mkubwa kwenye maeneo ambayo alishauriwa kufanyia mabadiliko, pia alikuwa mvumilivu jambo ambalo nimekumbushwa hapa, “ alisema
Aidha Rais Samia alisema Mzee Msuya alikuwa ni muumini wa kujenga umoja na mshikamano na kwamba ameacha alama hiyo hata pale Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Hata hivyo Rais Samia alisema Mzee Msuya, alikuwa na salamu mbili ambazo kila anapokutana naye ilikuwa ni lazima amuueleze ili aweze kuzitekeleza.
Rais Samia alisema mambo hayo ambayo marehemu Msuya alikuwa akimweleza hayatekeleze ni mradi wa maji Same-Mwanga-Korogwe na mradi wa barabara iliyopewa jina la
‘Cde Msuya Bypass’ na kusisitiza kuwa salamu hizo mbili zilimkeleleta Mzee Msuya na alitaka Rais azitekeleze.
“Mwaka 2024 Ikulu Dodoma nilifanya mkutano wa vyama vyote vya ushirika na bila kumwalika nilimkuta Msuya amekaa kitako, alikaa kimya wakati wa mkutano na ulipomalizika alihitaji kuniona na alifika ofisini kwangu na kunieleza aliyotaka kuniambia.
“Hata hivyo alikuwa na salamu mbili kubwa kwangu ambayo ni miradi mikubwa ilikuwa inamkereketa kwenye roho yake na alitaka niitekeleze, mara ya mwisho kwa faraja kubwa nilimuona pale Mwanga wakati wa ufunguzi wa mradi wa maji, kutembea hawezi lakini alikuwepo na kigari chake,” alisema Rais Samia
Alisema baada ya kusikia taarifa ya kifo cha Msuya alimshukuru Mungu kwa kuwa kimetokea wakati ambao tayari alikuwa ametimiza ahadi ya ujenzi miradi hiyo.
Kwa upande wake Rais mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete alisema Mzee Msuya alikuwa na uelewa mkubwa katika masuala ya fedha na uchumi, jambo ambalo lilimfanya kuaminiwa na kusimamia sekta ya uchumi katika vipindi vigumu nchini.
Dkt. Kikwete aliongeza kuwa wakati wa uhai wake mzee Msuya aliongoza Wizara ya Fedha wakati nchi ikiwa na uhaba wa bidhaa, uhaba wa fedha za kigeni kutokana na kudumaa kwa uchumi na uhaba wa upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii ikiwemo elimu, afya, maji na barabara.
Kwa mujibu wa Dkt. Kikwete, licha ya hali ya kiuchumi kutokuwa nzuri, mzee Msuya aliongoza kwa juhudi kubwa akizuia mambo yasiharibike zaidi.
Naye Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma alisema Mzee Msuya alikuwa tegemeo kubwa katika kipindi cha uongozi wa Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na alifanya kazi kwa moyo wa kujitoa katika kuleta maendeleo ya nchi licha ya Taifa kupitia changamoto kwa vipindi tofauti.
“Walimtegemea Mzee Msuya kwa sababu hakuwa mjeuri wala mkali bali alikuwa na ujasili, ushupavu na ustamilivu ambao aliutumia na kuleta Maendeleo makubwa katika nchi yetu, Hali yake hiyo ilimfanya apewe kazi zile ngumu ngumu zenye joto,” alisema Jaji Mkuuu
Writren by Janeth Jovin