Rais Samia atoa maelekezo matano upatikanaji Maji ya uhakika nchini

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo matano kwa Wizara ya Maji yanayolenga kuhakikisha huduma za maji safi katika maeneo mbalimbali nchini hasa ya mijini na Vijijini zinapatikana kwa uhakika.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo Machi 22,2025 jijini Dar es Salaam wakati akizindua Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002, toleo la 2025.
Moja ya maelekezo aliyoyatoa Rais Samia ameitaka Wizara hiyo kuimarisha usalama wa maji, kulinda miundombinu na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya mjini na vijijini.
Amesema pamoja na mambo makubwa yaliyofanyika amewataka wizara kuimarisha usalama wa maji nchini na kuhakikisha vyanzo vinavyotoa maji hayo vinalindwa.
”Kazi ya kulinda vyanzo vya maji si ya wizara ya maji peke yake, ni ya kila mtanzania tulinde vyanzo vyetu iwe vile vya katikati ya msitu, kwenye maziwa yetu na moja ya sifa ya kulinda vyanzo vyetu ni kulinda mazingira yetu kwa kutokata miti ovyo.
”Lakini pia tunapaswa kulinda miundombinu ile ambayo tumeijenga kwa gharama kubwa kupeleka maji kwa wananchi ili upatikanaji wa maji uwe wa usalama na uhakika , kwa sababu tukiruhusu mabomba yapasuliwe njiani hatujui nini kitaingia humo , hivyo kuna kazi kubwa ya kulinda miundombinu hiyo,” amesema Rais Samia
Aidha Rais Samia amesisitiza kuwa ni muhimu kulinda vyanzo na miundombinu hiyo ili wananchi wawe na uhakika wa upatikanaji wa maji
Hata hivyo Rais Samia amesema sera ya maji inabadilike kulingana na ongezeko la watu, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kiasi kikubwa yataathiri katika upatikanaji wa maji na vyanzo vya maji.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni suluhu ya tatizo la maji nchini kutokana na juhudi zake za kusimamia miradi ya maji na kuhakikisha huduma inawafikia wananchi wa mijini na vijijini.
Aweso amesema serikali imepiga hatua kubwa katika upatikanaji wa maji safi na salama katika kipindi hiki cha uongozi wake na kwamba hadi sasa, zaidi ya vijiji 12,500 vinapata huduma ya maji nchi nzima, na vimebaki vijiji 2,000 tu ambavyo navyo vinaendelea kufikiwa kupitia miradi mbalimbali.
Aidha, Aweso amesema zoezi la kuchimba visima zaidi ya 900 linaendelea, hatua itakayosaidia kupunguza uhaba wa maji na kuwahakikishia Watanzania upatikanaji wa maji safi na salama.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso ametoa wito kwa watumishi wa sekta ya maji kuwa waadilifu, akisisitiza kuwa ataendelea kusimamia haki na wajibu wao ili kuhakikisha wanatimiza lengo la Rais Samia la kutatua changamoto ya maji kwa Watanzania wote.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia (WB), Nathan Belete, amesema Tanzania imekuwa mfano bora kwa mataifa ya Afrika katika utoaji wa huduma za maji kutokana na usimamizi mzuri wa miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini.
Hata hivyo Belete ameipongeza Tanzania kwa kushinda tuzo mara mbili mfululizo kama nchi inayoongoza katika sekta ya maji barani Afrika, akisema kuwa ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine.
Written by Janeth Jovin