Rais Samia atoa sababu sekta ya habari kupelekwa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo
![](https://bongo5.com/wp-content/uploads/2024/12/IMG-20241210-WA0092-1536x951-1.jpg)
Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa moja ya sababu ya kuitoa sekta ya habari katika Wizara ya Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na kuipeleka Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo ni kuipa nguvu teknolojia ya habari.
Rais Samia ameyasema hayo leo Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua ambapo amesema teknolojia ya habari ilisahaulika huku nguvu kubwa ikiwekwa kwenye habari.
“Kwa kuwa tunakwenda na kasi ya ukuaji wa sekta ya mawasiliano na teknolojia na siyo tu hapa ndani ya nchi bali duniani nzima, pia kama unavyoona tuna mkakati wa uchumi wa kidigitali wa kitaifa ambao ukiutizama vizuri unataka shughuli ya peke yake.
“Sasa uzoefu wangu katika miaka hii mitatu nimeona nguvu kubwa inakwenda sekta ya habari na huku kwingine mnafanya vizuri lakini hatuendi kwa kasi ile inayotakiwa hivyo nimeitoa habari ili mjikite zaidi kwenye teknolojia ya habari,” amesema
Written by Janeth Jovin