Habari

Rais Samia awataka vijana, viongozi wa kisiasa kujifunza kwa hayati Sokoine

RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka vijana, viongozi wa kisiasa wa sasa na wajao kujifunza uaminifu, nidhamu na uchapakazi aliyekuwa nao Waziri Mkuu wa Zamani Hayati Edward Moringe Sokoine.

Rais Samia amesema kiongozi huyo alikuwa mwaminifu sana kwa mamlaka yake ya uteuzi na ndio maana alikasimiwa majukumu mengi na makubwa ikiwemo uwaziri Mkuu katika umri mdogo na kwamba katika hilo wanajifunza kuwa mtu akiwa mwadilifu na mchapakazi hana haja ya kukimbizana na vyeo bali vitamfuata ulipo.

Rais Samia ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu cha maisha na Uongozi wa Edward Moringe Sokoine kilichoandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

Amesema kuwa Waziri Mkuu wa Zamani Hayati Edward Moringe Sokoine alikuwa ni kiongozi aliyesimama imara katika kipindi mbacho nchi ilikubwa na changamoto za Kiuchumi, uhaba wa chakula na miundombinu duni.

“Kiongozi huyo alipenda maendeleo kwa watu aliowaongoza na Taifa kwa ujumla na kwamba alikuwa mtu ambaye licha ya kuishi na kuheshimu mila na desturi za kimasai hakukubali kupofushwa na desturi zinazorudisha nyuma maendeleo ya jamii yake.

“Tunamsoma Sokoine kama kiongozi aliyekuwa akiwahimiza watoto wa kimasai kutumia fursa za elimu na kwamba simulizi kuhusu maisha yake binafsi akiwa mdogo inatoa mwanga pia kuhusu namna alivyoishi hata ukubwani,” amesema

Amesema Sokoine alifanya maamuzi kwa kutumia taarifa sahihi hivyo hakuonea au kupendelea mtu na kwamba alikuwa baba wa mfano ambaye pamoja na majukumu yake ya kiuongozi hakuacha jukumu lake la kulea.

“Linapokuja suala la kiongozi tunamuona Sokoine kama kiongozi na mwanasiasa mzalendo na mwajibikaji, kitabu kikaonyesha jinsi sokoine alivyohudumu kwa welevu na uandilifu mkubwa katika nafasi zote za uongozi alizohudumu,” alisema

Amesema Sokoine alikuwa kiongozi aliendeleza kilimo, kufanya mageuzi katika uchumi kwa kuruhusu biashara huria ili kuweza kukidhi mahitaji ya wananchi kwa kuboresha huduma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na wake wa hayati Edward Moringe Sokoine kabla ya kuzindua Kitabu kinachohusu Maisha na Uongozi wake katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) leo tarehe 30 Septemba, 2024.

“Kitabu hiki hakiandiki historia mpya ya Sokoine kwani Sokoine alijiandikia historia yeye mwenyewe, kitabu kinajaribu kuweka pamoja mapito ya kiongozi wetu huyu wakati akijiandikia historia yake.

“Kitabu hiki ni hidaya kwa watanzania kwa hiyo yapo mafunzo mengi sana kwa viongozi wa sasa na wanaochipukia kupitia kitabu hiki tunapata fursa ya kumfahamu sokoine kupitia maisha yake binafsi tangu alipozaliwa haki kushika madaraka makubwa zaidi nchini,” alisema

Aidha amesema kitabu hicho kimeweka kumbukumbu ya kina ya maisha ya kiongozi huyo na kitambua mchango wake kwenye ujenzi wa taifa hili na kwamba kupitia maisha ya Sokoine wanapata uelewa na fursa ya kujua mapito ya nchi kwa undani zaidi.

Naye Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amesema uandishiwa kitabu baada ya kiongozi kufarikini mgumu na hiyo inatokana na ukweli kwamba baadhi ya taarifa binafsi zisizoandikwa siyo rahisi wengine kuzifahamu .

“Ninawaomba viongozi ambao Mungu amewajalia uhai hadi sasa wajitahidi kuandika tahasifu zao wakingali hai, aidha Rais ninaomba serikali yao ione uwezekano wa kuwawezesha viongozi wetu wastaafu fedha na rasilimali watu ili waweze kufanya kazi hiyo ya kuandika tawasifu zao,” amesema

Kwa Upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema Sokoine alikuwa ni kiongozi aliyepambana kwa dhati dhidi ya rushwq na uhujumu uchumi hivyo amewataka viongozi wa umma kukisoma kitabu hicho ili waweze kujifunza utendaji bora wa kiongozi huyo.

Amesema maono na fikra za Sokoine zinatoa mwanga wa kuelewa siasa za hapa nchini na Afrika kwa ujumla na kwamba kiongozi huyo alijenga nidhamu ya utendaji ndani ya serikali.

“Kupitia kitabu hiki tutapata fursa ya kujifunza kuhusu kazi, changamoto na maisha kwa ujumla ya Sokoine ambaye alikuwa kiongozi mzuri na mfano wa kuigwa katika utumishi wake, “ alisema Simbachawene

Writen by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents