Habari

Rais wa Afrika Kusini ampigia simu Musk kutuliza maneno juu ya sheria mpya ya ardhi

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amechukua hatua ya kumaliza mzozo kati yake na utawala mpya wa Marekani kuhusu sheria mpya ya ardhi kwa kuzungumza na Elon Musk.

Musk ni mshauri wa karibu wa Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye siku ya Jumapili alitishia kusitisha ufadhili kwa siku zijazo kwa Afrika Kusini kwa madai kuwa inanyakua ardhi na “kuwatendea vibaya watu wa tabaka fulani.”

Bilionea huyo wa teknolojia mzaliwa wa Afrika Kusini alichapisha ukosoaji wake kupitia X, akiuliza kwa nini Ramaphosa ana “sheria za wazi za ubaguzi wa rangi katika umiliki wa ardhi.”

Ofisi ya Ramaphosa imesema katika mazungumzo ya simu ya rais na Musk, “rais alisisitiza maadili ya Afrika Kusini yaliyopo kikatiba ni ya kuheshimu utawala wa sheria, haki, na usawa”

Mwezi uliopita, Rais Cyril Ramaphosa alitia saini sheria inayoruhusu unyakuzi wa ardhi bila fidia katika sababu fulani.

Umiliki wa ardhi kwa muda mrefu umekuwa suala la kutatanisha nchini Afrika Kusini huku mashamba mengi ya binafsi yakimilikiwa na watu weupe, miaka 30 baada ya kumalizika kwa mfumo wa kibaguzi wa ubaguzi wa rangi.

Kumekuwa na wito wa mara kwa mara kwa serikali kushughulikia mageuzi ya ardhi na kukabiliana na dhuluma za zamani za ubaguzi wa rangi.

Katika majibu yake ya awali kwa Trump, rais wa Afrika Kusini amesema “serikali yake haijamnyang’anya ardhi yoyote.”

Siku ya Jumapili, Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social: “Nitakata ufadhili wote wa siku zijazo kwa Afrika Kusini hadi uchunguzi kamili wa hali hii ukamilike!”

Sheria mpya ya Afŕika Kusini inaruhusu unyakuzi wa ardhi bila fidia katika hali ambapo ni “haki na ni sawa kwa maslahi ya umma” kufanya hivyo.

Hii inajumuisha ikiwa ardhi haitumiki na hakuna nia ya kuiendeleza au haizalishi pesa, au ikiwa inahatarisha usalama wa watu.

Mwaka 1913, utawala wa kikoloni wa Uingereza ulipitisha sheria iliyozuia haki ya kumiliki ardhi kwa watu weusi ambao ndio wengi nchini humo.

Sheria hiyo ilifanya sehemu kubwa ya ardhi kuwa chini ya udhibiti wa Wazungu walio wachache na kuondolewa kwa lazima watu weusi katika ardhi zao na kupelekwa katika vitongoji maskini kwa miongo kadhaa hadi mwisho wa ubaguzi wa rangi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents