Habari

Rais wa Zanzibar avutia washiriki ‘NMB 5K Run 2021’

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameongoza mamia ya wakimbiaji walioshiriki mbio za kilomita 5 za ‘NMB 5K Run 2021, zilizodhaminiwa na Benki ya NMB, ambapo ushiriki wake uliwavutia wengi zaidi miongoni mwa waliojitosa katika Zanzibar International Marathon 2021.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Huseein Mwinyi na Mke wake Mama Mariam, Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid  Mwita ( wa kwanza kulia) na Kaimu Afisa Mkuu Ukaguzi wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa (kushoto) wakishiriki mbio za Kimataifa za Zanzibar Marathon za Kilomita tano zilizodhaminiwa na Benki ya NMB zilizofanyika jumapili visiwani Zanzibar

NMB 5K Run 2021 zilikuwa ni sehemu ya Zanzibar International Marathon – mbio zilizo fanyika chini ya kaulimbiu ya ‘Tunakuza Uchumi wa Bluu Kupitia Michezo Zanzibar, zilizoanzia Ngome Kongwe na kuishia Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar, ambako Dk. Mwinyi alikuwa mmoja wa waliokimbia kilomita 5.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Huseein Mwinyi na   Mke wake Mama Mariam na Kaimu Afisa Mkuu Ukaguzi wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedcto Baragomwa (kushoto) wakishiriki mbio za Kimataifa za  Zanzibar Marathon za Kilomita tano zilizodhaminiwa na Benki ya NMB. Mbio hizo zilifanyika visiwani Zanzibar juzi.

NMB ilidhamini kilomita 5 kwa Sh. Milioni 35, lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya Zanzibar katika kuhamasisha na kukuza utalii, kukuza Uchumi wa Bluu na kuchagiza jamii kudumisha utamaduni chanya wa kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukizwa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Husein Mwinyi,  Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman (kushoto) na Kaimu Afisa Mkuu Ukaguzi wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedcto Baragomwa (katikati) wakishiriki mbio za Kimataifa za  Zanzibar Marathon za Kilomita tano zilizodhaminiwa na Benki ya NMB na kufanyika juzi visiwani Zanzibar.

Akizungumza kabla ya kukabidhi medali na zawadi kwa washindi wa kilomita 5, 10, 21, watoto, walemavu na wagonjwa wa afya ya akili walioshiriki mbio hizo, Rais Mwinyi aliwashukuru waratibu, lakini akawapongeza wadhamini, wakiwamo NMB kwa kuzirejesha mbio hizo zilizofanyika kwa mara ya mwisho miaka 10 iliyopita.

Watoto  nao pia walishiriki mbio  za Kimataifa za  Zanzibar Marathon za Kilomita tano zilizodhaminiwa na Benki ya NMB na kufanyika juzi visiwani Zanzibar.

Alisema waratibu na wadhamini wameonesha dhamira ya dhati ya kushirikiana na Serikali yake katika kukuza uchumi, kuhamasisha utalii na kuhimiza mazoezi ya viungo, huku akiitaja marathon hiyo kama chachu ya uibuaji na uendelezaji wa vipaji vya riadha vitakavyoitangaza Zanzibar kimataifa.

Watu mbali mbali walishiriki mbio za Kimataifa za  Zanzibar Marathon za Kilomita tano zilizodhaminiwa na Benki ya NMB na kufanyika juzi viziwani  Zanzibar.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mkuu Ukaguzi wa Ndani wa NMB – Benedicto Baragomwa, alisema benki yake inajisikia fahari kuwa mdhamini, na kwamba kutokana na NMB kuwa mdau mkubwa wa maendeleo, haikuwa ngumu kwao kufanya uamuzi wa kujitosa Zanzibar International Marathon.

NMB iliaahidi kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kila hatua inayolenga kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Taifa.

Related Articles

Back to top button