Habari

RC Iringa Queen Sendiga atoa taarifa rasmi za mkoa wake

Akiongea na wana habari Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mh Queen Sendiga akizungumza wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya kongamano la uwekezaji kwenye sekta ya misitu.amesema kuwa:-

“Mkoa wa Iringa ni kati ya mikoa 31 ya Tanzania ambao una eneo la kilomita za mraba 35,743 sawa na maili za mraba 13,800 ikiwa na jumla ya idadi ya watu wanaokadiriwa kuwa milioni 1.5 ambao shughuli zao kubwa za kiuchumi zinahusisha kilimo ikiwemo misitu ambayo inatoa mchango mkubwa kwenye mapato ya Serikali.

shughuli za upandaji miti katika mkoa wetu zilianza zamani, mwanzoni mwa miaka ya 1970, Serikali ilipoanzisha shamba la Saohil ambalo ndio shamba kongwe zaidi hapa nchini lenye ukubwa wa hekari 60,000. Historia na uzoefu wa upandaji miti umewavutia makampuni na wananchi kuwekeza katika sekta hii ya misitu kwenye mkoa wetu na mikoa jirani. Inakadiriwa misitu ya kupandwa hapa nchini kwetu inafikia eneo la hekari takribani 325,000. Zaidi ya asilimia 40% ya eneo hilo zinapatikana katika Mkoa wa Iringa. Hii pia inatokana na ukweli kwamba Mikoa ya nyanda za juu kusini imejaliwa kuwa na hali nzuri ya hewa inayoruhusu ukuaji mzuri wa miti ikiwa ni pamoja na mvua za kutosha, hali nzuri ya hewa na ardhi inayoruhusu miti ya kupanda kukua kwa haraka. Kutokana na hali hizi nzuri, Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuwavutia kwa kiasi kikubwa wawekezaji katika upandaji, uchakataji na watoa huduma katika sekta ya misitu. Hata hivyo, bado zipo fursa nyingi sana za kuwekeza. Mkoa una kiu kubwa kuona uwekezaji katika misitu unakua na kuchangia zaidi katika pato la taifa. Kwasasa misitu inachangia asilimia 75% ya mapato katika mkoa wetu.

Kwa ujumla, uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani katika sekta hii ya misitu bado uko chini sana kulinganisha na fursa zilizopo. Wawekezaji wengi wamejikita katika uzalishaji wa mbao, nguzo, pamoja na bidhaa zilizohandisiwa (engineered wood products) kama vile plywood. Lakini zipo fursa zaidi ya hizi kama vile uzalishaji wa karatasi ambazo zinatumika sana katika shule zetu, samani zenye ubora zinazoweza kushindanishwa katika masoko ya ndani na ya nje, utengenezaji wa viberiti, toothpicks pamoja na bidhaa nyingine nyingi. Sambamba na hili, uchakataji wa mbao umekuwa ukifanyika kwa kutumia teknolojia duni zonazopunguza ufanisi na kusababisha upotevu wa malighafi. Katika hili, zipo fursa za utengenezaji na uuzaji wa mashine ama teknolojia mbadala za uchakataji wa mazao ya misitu ili kuongeza ufanisi na faida. Yapo maeneo ambayo uwekezaji katika uchakataji wa bidhaa za misitu haukuyafikia japokuwa mali ghafi zipo za kutosha. Hii kwa kiasi flani inatokana na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu fursa hizo. Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na barabara za vijijini ili wawekezaji waweze kuzifikia mali ghafi zilizopo na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika mkoa wetu. Hivyo, ipo nafasi kubwa ya kupanua wigo wa aina za bidhaa za misitu na ufanisi katika uchakataji, teknolojia mbadala zinazo zalisha bidhaa mbali mbali za mazao ya misitu ikiwa ni pamoja na utumiaji wa mabaki kutengeneza bidhaa hizo na kuboresha upatikanaji wa masoko.

 

Aidha, pamoja na kuwa uzalishaji wa bidhaa za mbao zilizohandisiwa (EWP) unatiliwa mkazo zaidi katika mkoa wa Iringa kutokana na ufanisi mkubwa na matumizi mazuri ya mali ghafi itokanayo na misitu,  bado ipo fursa ya uwekezaji katika uzalishaji wa karatasi nyeupe, karatasi za vifungashio, veneer, marine Boards, MDF, Particle Boards, wood chips, block boards na bidhaa nyingine za kundi hilo. Nawakaribisha sana kuwekeza na kuja kujifunza kwenye kongamano kuhusiana na maeneo haya muhimu ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi katika sekta za ujenzi na fenicha.

Katika kuonesha fursa zilizopo na kuongeza chachu ya uwekezaji katika sekta ya misitu mkoani Iringa, mkoa kwa kushirikiana na taasisi zinazojihusisha na shughuli  za misitu kama Taasisi ya Uendelezaji Misitu Tanzania (Forestry Development Trust – FDT), m\Mradi wa Panda Miti Kibiashara Awamu ya pili (Participatory Plantation Forestry Programme – PFP 2) pamoja wa wadau wengine katika sekta hii ya misitu wameandaa Kongamano la Uwekezaji katika Sekta ya Misitu mkoani Iringa.  Kongamano hilo litafanyika kuanzia tarehe 10th mpaka 12th Novemba 2021 katika viwanja vya shule ya msingi Wambi mjini Mafinga. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa atakayetufungulia kongamano hilo, na matarajio ni kwamba kongamano hili litakuwa endelevu ambapo litafanyika kila mwaka.

Kongamano hili linatarajiwa kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya misitu kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na sekta zinazotoa huduma kwenye misitu, wawekezaji wa sekta ya misitu, watunga sera, taasisi na wizara zinazohusika na misitu na uwekezaji (OR TAMISEMI, Wizara ya Maliasiri na Utalii, Wizara ya Uwekezaji, wizara ya viwanda na biashara, kituo cha uwekezaji – TIC,) wazalishaji na wasambazaji wa teknolojia za uchakataji wa mazao ya misitu, taasisi za elimu ya misitu, wadau katika usafirishaji, taasisi za fedha, pamoja na wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa sekta ya misitu. Kongamano litakuwa na mijadala mbali mbali na maonyesho ya fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya misitu, teknolojia za uchakataji wa mazao ya misitu pamoja na kazi zinazofanywa na wazalishaji waliokwisha wekeza katika misitu. Pia kutakuwa na safari za kutembelea maeneo ya uwekezaji uliofanyika katika misitu kwa lengo la kujifunza zaidi.

 

Kuandaliwa kwa kongamano hili ni sehemu ya utekelezaji wa maelezo ya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa tarehe 22 April 2021 alipolihutubia bunge ambapo alisisitiza kuanzisha na kuendeleza viwanda katika maeneo ambayo malighafi zinapopatikana, na kutenga maeneo huru na kongani za kibiashara. Aidha, ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ibara ya 69 (E, F na G) inayoelekeza kuendeleza sekta ya misitu kwa manufaa ya Taifa letu. Washiriki wanaweza kuhudhuria moja kwa moja au kwa njia ya mtandao (live streaming).

Hivyo basi, Kongamano hili la uwekezaji katika mkoa wa Iringa ni mwendelezo wa  juhudi mbalimbali zinazofanywa na mkoa katika kuchochea uwekezaji. Aidha,  linatarajiwa kuvutia wawekezaji wapya wazawa na wa kutoka nje ya nchi na pia kuongeza kasi ya uwekezaji endelevu katika sekta ya misitu kuanzia kwenye upandaji miti wenye tija  na uzalishaji wa mazao ya misitu kwa kuzingatia nmnyororo wa thamani ili kupata maendeleo endelevu.

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents