Habari

Racheal: Gofu imenifanya nimepanda ndege kwa mara ya kwanza, umebadilisha maisha ya familia yangu

Mchezaji wa Gofu kutoka klabu ya Kilimanjaro, Racheal Mushi amesema kuwa kupitia mchezo wa gofu amepata mafanikio makubwa ikiwemo ya kupanda ndege kwa mara ya kwanza.

Mushi ameyasema hayo hivi karibuni wakati  wa mashindano ya Lina PG Tour msimu wa tatu yaliyorindima katika Viwanja vya TPC Moshi mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kumuenzi mchezaji gofu wa zamani timu ya Taifa ya wanawake marehemu Lina Nkya.

Amesema toka ameanza kucheza gofu mpaka sasa anashukuru kwani mchezo huo umemuwezesha kwenda nchi za nje, kukutana na watu tofauti tofauti pamoja na kubadilisha maisha ya familia yake kutoa hatua moja kwenda nyingine.

“Ki ukweli kupitia gofu nilipanda ndege kwa mara ya kwanza kwenda nchi za nje kushiriki mashindano, lakini mchezo huu umesaidia kwa kiasi kikubwa kubadilisha maisha katika familia yangu katika hilo namshukuru sana Mungu, niwaombe watanzania hasa vijana kujitokeza kwa wingi kucheza mchezo huu.

“Mchezo huu si wa matajiri kama wanavyosema watu wengine bali kila mtu anaweza kucheza cha muhimu ni kufanya mazoezi kwa wingi na kuweka juhudi bila kukata tamaa, ukiyafanya hayo utafika mbali,” amesema Mushi

Aidha Mushi amewapongeza waandaaji na wadhamini wa mashindano ya Lina PG Tour na kusema kuwa ni moja ya michuano ambayo imekuwa ikiwaweka fiti kuweza kushiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

“Tunawashukuru sana walioandaa mashindano haya ya Lina PG Tour, tunaendelea kuwaombea waendelee kutuleta michuano hii ambayo kiukweli imekuwa ikutuandaa vema na kuleta ushindani mkubwa kwa wachezaji wengi, chipukizi na wakulipwa, tunawaomba wadau wengine wajitokeze kuweza kusapoti ili kuhakikisha wachezaji wanapata mashindano mengi zaidi,” amesema

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents