Rwanda yatengeneza programu maalum ya kutambua wenye corona

Rwanda wametengeneza Programu(app) ambayo inaweza kuhifadhi habari kuhusu watu wanaoingia katika maeneo ya umma, ili kurahisisha kazi ya mamlaka ya afya kutambua watu waliokutana na mtu aliyeambukizwa virusi vya Corona.

Muanzilishi wa programu hiyo, Bi Jeanne Bovine Ishemaryayo anasema kuwa mamlaka iliruhusu matumizi ya programu yake ambayo sasa inatumika katika baadhi ya makanisa ,masoko na sehemu nyingine zenye mkusanyiko wa watu.

Programu hii ni mbadala wa daftari , maeneo mengine watu walikuwa wanandika majina kwa ajili ya kuingia mahali fulani.

covid

Katika kanisa la Anglicana mjini Kigali,wakristo wakiwa wanaingia mmoja baada ya mwingine,kwa uangalifu wa afisa mmoja wa kanisa ,Obed Kwizera:

”Kila mtu anabonyeza kadi yake kwenye kifaa hiki. sisi tunabaki na wasifu wa kila mkristo kiasi kwamba likitokea tatizo lolote tunaingia katika data na kupata taarifa zote za kila mtu.Sisi tunakuwa na wakristo takriban elfu mbili wanaohudhuria misa kila Jumapili ,ni rahisi wakitumia hii kadi badala ya sisi kuandika utambulisho wao kwenye daftari.”

Kutokana na ugonjwa wa Covid19 Sehemu za umma hapa nchini Rwanda zimekuwa zikitakiwa kurekodi vitambulisho vya msingi vya kila mtu ,ili kama kutakuwa na mgonjwa mamlaka husika ziweze kufahamu njia zote alizopitia na watu aliokutana nao.Katika sehemu nyingi kazi hii hufanywa kwa kuandika utambulisho wa mtu kwenye vitabu au daftari .

Bi Ishemaryayo mhandisi wa teknolojia anasema alibuni programu hiyo ili kutatua shida hiyo:

Programu ya kugundua mwenye corona
”kadi hii ya kielectroniki inasaidia kunakili na kuhifadhi data za kila mtu hususan katika sehemu za mikusanyiko bila kulazimika kutumia daftari au karatasi.Na hii inaweza kusaidia mamlaka zinazopambana na Covid 19 kufahamu jinsi ugonjwa huo unavyosambaa sehemu mbali na kutambua kwa urahisi watu waliokutana na mgonjwa”

Kutokana ongezeko la maambukizi ,serikali imekuwa ikiamua kufunga shughuli mbalimbali pamoja na kuwataka wananchi kubaki majumbani(Lockdown) na wakati fulani masoko makuu mawili katikati ya mji wa Kigali yaliamurishwa kufunga milango baada ya baadhi ya wachuuzi kuambukizwa.

Jeanne Bovine Ishemaryayo ,mwenye umri wa miaka 27 anasema kutokana na kadi yake kwa sasa hakuna haja ya kufunga mahali penye mkusanyiko kama soko :

”Labda nitoe mfano tu : wa wakati serikali iliamua kufunga masoko mjini .Pengine masoko hayo yasingelifungwa kwani Baada ya kutambua walioambukizwa Covid, kadi hii ingelitumiwa kujua mgonjwa huyo alipitia soko gani na wachuuzi aliokutana nao au hata kama ni mchuuzi aliyepatikana na Covid ingelikuwa rahisi kutambua watu aliokutana nao ,na masoko yakaendelea kufanya kazi”

Japo jiji la Kigali sasa linashuhudia kipindi kingine cha marufuku ya kutoka nje kwa wakazi wake , masoko bado yanafanya kazi na katika baadhi ya masoko programu yake inatumiwa.

Related Articles

Back to top button