
Aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne leo Jumatatu Juni 20,2022 watafikishwa tena katika mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kusikiliza tuhuma mbalimbali zinazowakabili ikiwemo uhujumu uchumi.
Kesi hiyo namba mbili ya mwaka 2022 inasikilizwa na hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Salome Mshasha na mawakili wanne kutoka upande wa jamhuri ambao ni Tumain Kweka, Khalili Nuda, Verediana Mteuza na Suzy Kimaro.
Juni 7, 2022 hakimu Mshasha aliahirisha kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika ambapo Sabaya na wenzake walirudishwa katika gereza la Karanga.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Sylvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey.
Hata hivyo Juni 7,2022 wakati kesi hiyo ilipoitwa kutajwa wakili wa upande wa utetezi, Hellen Mahuna aliiomba mahakama hiyo kuharakisha upelelezi kwa kuwa mteja wake ambaye ni Sabaya ni mgonjwa kutokana na uvimbe alionao kichwani ambao anatakiwa kufanyiwa upasuaji.
Chanzo cha habari Mwananchi.