Michezo

Samatta kuikosa Burundi leo

Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” leo atakuwa na jaribio jingine la kuwakabili Burundi ‘Intamba Murugamba’ katika mchezo wa kimataifa wa Kirafiki uliopo kwenye kalenda ya FIFA.

Mchezo huo utakuwa ni wa Pili kwa kocha Mayanga ambaye Jumamosi iliyopita alianza vizuri kibarua chake kwa kuifunga Botswana mabao 2-0 kwenye mechi ya Kirafiki.

Burundi tayari wamewasili Dar es Salaam jumapili mchana wakiwa na kikosi chao kamili kikiongizwa na Mshambuliaji wa Simba Laudit Mavugo.

Kocha Mayanga katika mchezo wake wa leo atakosa huduma ya Mshambuliaji wake Mbwana Samatta anayoichezea KRC Genk ya Ubelgiji ambaye alifunga mabao yote mawili kwenye mchezo uliopita.

Mayanga amesema amemruhusu Samatta kuondoka ili kutumia kikosi chake cha wachezaji wanacheza ligi ya ndani, lengo ni kuiandaa timu ambayo itashiriki fainali za CHAN ambazo zinashirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani kwao.

Mayanga amesema maandalizi yote kuelekea mchezo wa kesho yamekamilika na anatarajia kupata ushindi mwingine kutokana na uelewano mzuri waliokuwa nao wachezaji wake.

“Najua utakuwa mchezo mzuri wenye ushindani kwa kuwa Burundi ni majirani zetu, tunajuana lakini naamini tutashinda kutokana na maandalizi mazuri tuliyokuwa nayo kuelekea mchezo huo,” amesema Mayanga.

Kocha huyo amesema kutokuwepo kwa Samatta kwenye mchezo huo hakutaiathiri timu yake kwani kuna wachezaji wengi ambao wanaweza kucheza nafasi yake.

Amesema kwenye nafasi hiyo anaweza kumtumia Abrahmani Mussa wa Ruvu Shooting kucheza sambamba na Ibrahim Ajibu na anaamini atafanya vizuri kutokana na uwezo aliokuwa nao mchezaji huyo.

Amesema kama ilivyokuwa kwenye mchezo uliopita mchezo wa kesho atatumia mfumo ule ule wa 4-4-2 kwa sababu wanataka kushambulia zaidi na kufunga mabao mengi.

Nahodha wa Burundi Mavugo amesema mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa sababu Tanzania wanakikosi imara ambacho kinaundwa na wachezaji wengi vijana lakini ameahidi kupata ushindi kwenye mchezo huo.

“Tumekuja tukiwa na kikosi imara ambacho kina wachezaji wengi wenye uzoefu kwa hiyo pamoja na kucheza ugenini lakini naamini tutafanya vizuri,” amesema Mavugo.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa mwaka 2014 uwanja wa Taifa Dar es Salaam na Tanzania kufungwa mabao 3-1.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents