Technology

Sekta ya mawasiliano ya simu inavyopunguza umaskini nchini Tanzania

Toka mwaka 2016 Serikali ya Tanzania imekuwa ikiweka juhudi kubwa katika utekelezaji wa mkakati wake wa kuibadili Tanzania kuwa nchi ya viwanda ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Mojawapo ya malengo ya Dira ya Maendeleo ni kutengeneza uchumi shindani na imara wenye faida kwa wote.

Hili ni jambo muhimu, kwamba lazima tuhakikishe maendeleo yoyote yanayopatikana kwa taifa letu yananufaisha Watanzania wote.

Moja wa wadau wa maendeleo nchini ni shirika la World Vision ambao wanaeleza kwamba iko tofauti kubwa ya maendeleo kati ya maeneo ya vijini na mijini.

Wanashauri kwamba moja ya namna ya kubadili hali ya maisha kwa wakazi wa vijijini ni kujenga mfumo wa vikundi vya kuweka akiba vya watu thelathini kwa kundi.

Vikundi hivi husaidia watu kuweka akiba lakini pia kujenga uwezekano wa kupokea na kutoa mikopo.

Mbali na kujengea wananchi mazingira ya kuweza kukopesheka, serikali pia imejitahidi kuhakikisha watu wa vijijini wanapata nishati ya umeme. Kufikia mwaka 2022 serikali inakusudia kuwa imeunganisha vijiji zaidi ya 7,800 kupata umeme.

Katika siku za karibuni, maendeleo ya teknolojia na kampuni za mawasiliano ya simu yamekuwa sehemu muhimu sana ya kusaidia kukuza kipato na kuondoa tofauti za kiuchumi kati ya miji na vijiji.

Huduma za mawasiliano, kutuma na kupokea fedha na hata mtandao wa intaneti ambazo zilikuwa ni kwa watu wa mijini tu sasa zinapatikana kwa kila Mtanzania popote alipo kupitia simu yake ya mkononi.

Zipo huduma nyingine nyingi zaidi kupitia simu, mfano wapo wakulima vijijini ambao sasa ni rahisi kujua hata bei za mazao kwenye masoko mijini kwa kutumia simu zao na hii ni faida kwao.

Zipo hata huduma za bima ya afya kupitia simu ya mkononi ambapo zinasaidia watumiaji wake kupata huduma bora za afya na kuwa uhakika hasa maeneo ya vijiji.

Ama kwa hakika sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi imeboresha maisha ya Watanzania na kupunguza pengo la maendeleo kati ya wakazi wa mijini na vijijini.

Hata hivyo changamoto bado zipo, kwani maendeleo haya bado yanafikia watu wachache tu na ni lazima kuwekeza zaidi katika miundombinu ya mawasiliano.

Lakini ili uwekezaji huu uweze kufanikiwa lazima kuendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji. Tuendelee kujenga vyema sekta hii ili faida zake ziweze kumfikia kila Mtanzania kwa ubora zaidi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents