Habari

Serikali ya Marekani na Serikali ya Tanzania Washiriki Mapambano Dhidi ya Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa

Dkt Ronald Benju kutoka Maabara ya Vetinari Tanzania akionyesha njia bora ya kutoa chanjo ya mbwa wakati wa maadhimisho ya Kichaa cha Mbwa duniani ambayo yamefanyika Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza mwishoni mwa wiki. Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), kupitia mradi wa Breakthrough ACTION kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Sehemu ya Afya Moja, Wizara za Mifugo, Afya, na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), walitumia fursa ya maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa kama sehemu ya juhudi za kimataifa za kupambana na ugonjwa huo kwa kupitia kampeni ya Kitaifa ya “Holela-Holela Itakukosti,” yenye lengo la kuiwezesha jamii kupambana na ugonjwa wa kichaa cha Mbwa. Mwenye kushika mbwa ni Afisa Mwelimishaji na ushauri tiba Mkoa wa Mwanza Colman Edward.

Misungwi, Mwanza Jumanne 1 Oktoba 2024 Katika maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani, Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wake wa Breakthrough ACTION, na Serikali ya Tanzania, ikiwakilishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Sehemu ya Afya Moja, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), wanaongoza juhudi za pamoja kulinda jamii zilizo hatarini dhidi ya tishio hatari la ugonjwa wa kichaa cha mbwa. Mikakati yao kabambe inazingatia elimu, programu za chanjo, na ushirikishwaji wa jamii, kwa lengo la kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa na kulinda afya ya binadamu na wanyama.

Kichaa cha mbwa bado ni changamoto kubwa ya afya ya umma nchini Tanzania, na husababisha vifo vya takribani watu 59,000 duniani kila mwaka, huku idadi kubwa ya vifo hivyo ikitokea barani Afrika. Ugonjwa huu, ambao kwa kiasi kikubwa huambukizwa kupitia kuumwa na wanyama wenye maambukizi, hasa mbwa, ni tishio kubwa kwa jamii zisizo na elimu ya afya ya umma na huduma za mifugo.

Daktari Stanford Ndibalema, Mkurugenzi Msaidizi Afya ya jamii ya Veterinari kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kupambana na kichaa cha mbwa. “Ushirikiano kati ya USAID na serikali ya Tanzania ni muhimu katika vita yetu dhidi ya kichaa cha mbwa. Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kuhakikisha kuwa jamii zinapewa elimu kuhusu hatari za ugonjwa huu na pia kupewa uwezo wa kuchukua hatua madhubuti za kujilinda wao wenyewe na wanyama wao,” alisema. Dkt. Ndibalema alisisitiza haja kubwa ya kampeni za chanjo na uhamasishaji wa jamii, akibainisha kuwa “kila mbwa aliyepatiwa chanjo ni hatua muhimu kuelekea jamii isiyo na kichaa cha mbwa.”

Sambamba na maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani, miradi ya USAID inalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu kichaa cha mbwa, umuhimu wa kuwachanja wanyama wao wa kufugwa, na hatua zinazopaswa kuchukuliwa endapo mtu ameng’atwa na mnyama hasa mbwa. Kampeni ya “Holela Holela Itakukosti,” ambayo tafsiri yake ni “uzembe ni gharama,” inahimiza uchanjaji wa mbwa na uwajibikaji wa wamiliki wa mbwa ili kupunguza maambukizi ya kichaa cha mbwa ndani ya jamii. Revina, mama wa watoto watatu kutoka Mwanza, alielezea uzoefu wake, “Kabla ya kampeni, sikuwa najua jinsi kichaa cha mbwa kilivyo hatari. Tulipojifunza umuhimu wa kuwachanja mbwa wetu, tulichukua hatua mara moja. Sasa, ninahisi salama zaidi kuwaacha watoto wangu kucheza nje.” Viongozi wa mitaa na wahudumu wa afya wamehamasishwa kufanya programu za uhamasishaji, kuhakikisha kuwa hata maeneo ya mbali kabisa yanafikiwa na taarifa muhimu na rasilimali zinazohitajika.

Wakati USAID na Serikali ya Tanzania wakiadhimisha Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani, dhamira yao ya kuzilinda jamii zilizo hatarini inaonekana wazi. Juhudi za pamoja kati ya USAID, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, na mashirika ya ndani zinaonyesha njia ya pamoja ya kukabiliana na ugonjwa unaozuilika lakini wenye athari kubwa. Kwa pamoja, wanakusudia sio tu kuondoa kichaa cha mbwa, bali pia kujenga jamii zenye afya na usalama kwa Watanzania wote.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents