Serikali yatoa Bilioni 4.2 kwa ajili ya uendeshaji Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Carolyne Nombo amesema kuwa hadi kufikia mwaka huu wa fedha 2025/2026 Serikali imetenga kiasi cha Bilioni 4.2 katika kipindi cha miaka minne ili kuendeleza Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.
Nombo ameyasema hayo jana wakati wa hafla ya utoaji tuzo hiyo jijini Dar es Salaam ambapo amesema fedha hizo zinetumika kugharamia uendeshaji wa jumla wa tuzo hiyo kila mwaka, Uchapishaji wa vitabu vilivyoshinda na utoaji wa zawadi kwa washindi.
Amesema uwekezaji huo wa fedha si tu umeongeza hamasa ya uandishi bunifu bali umeendelea kusaidia kukuza sekta ya uandishi na uchapishaji wa vitabu nchini.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia Wizara rasilimali fedha kwa ajili ya uendeshaji wa tuzo hii,” amesema
Aidha amesema kwa miaka ijayo Wizara inapanga kushirikiana na vyuo vikuu na wadau wa fasihi kuandaa warsha kwa waandishi chipukizi pamoja na kongamano la kitaifa la uandishi bunifu ili kuongeza ubunifu na hamasa ya Uandishi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Aneth Komba amesema uandishi bunifu ni nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo ya elimu nchini.
Amesisitiza kuwa sera ya elimu inalenga kukuza stadi za kusoma, kuandika na kuwasiliana kwa ufasaha kwa lugha ya Kiswahili pamoja na kuthamini utamaduni wa kitanzania.
“Uandishi bunifu unachangia kujenga fikra makini, uwezo wa kuchambua na kutatua changamoto pamoja na kuimarisha maadili na Umoja wa kitaifa,” amesema Komba
Komba amesema uandishi bunifu unasaidia wanafunzi kujiamini na kuboresha stadi za msingi za kujifunza.
Written by Janeth Jovin








