Michezo

Siioni nafasi ya kocha Pablo Franco Simba SC

Novemba 6, 2021 miamba ya soka Afrika Mashariki na Kati Simba SC ilimtambulisha rasmi kocha wake mpya raia wa Hispania Pablo Franco Martin kuchukua mikoba ya Didier Gomes Derosa.

Wakati Simba SC inampatia kandarasi ya miaka miwili, Pablo Franco ilijiwekea malengo mama kama klabu na hata kocha huyo akielezwa matamanio hayo ya timu.

Malengo hayo hayakuwa siri mara kadhaa viongozi wa Simba wamekuwa wakiyatamka hadharani na yakiwa kama sehemu ya makubaliano yao na Mhispania huyo.

Miongoni mwa malengo hayo ni kuhakikisha Simba SC inaingia hatua ya Nusu Fainali Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Pili kuutetea na kushinda Ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Katika malengo haya Pablo hajafanikiwa kuifikisha Simba Nusu Fainali ya Shirikisho Afrika baada ya kutolewa na Orlando Pirates kwa mikwaju ya penati 4-3 baada ya (Agg: 1-1).

Lakini pia nafasi ya Simba SC kushinda Ubingwa wa Ligi Kuu ni ndogo mno ukilinganisha na mtani wake Yanga SC ambaye anapewa nafasi kubwa hasa kutokana na wingi wa point walizoachwa Msimbazi na vijana wa msimbazi.

Mpaka hapo nafasi ya Pablo Franco kukinoa kikosi cha Simba SC ipo mashakani na huenda ikaamuliwa na Darby hii ya Kariakoo Aprili 30, 2022 hasa kama matokeo yatakuwa mazuri zaidi kwa upande wake.

Katika Ligi ya ndani Simba SC haioneshi uwezo wa kushinda kombe la Ligi Kuu msimu huu 2021/22. Wakati Yanga imekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu, ikionesha nia ya dhati ya kuutaka ubingwa baada ya kuukosa misimu minne mfululizo.

Kikosi cha Yanga kimekuwa na matokeo mazuri kila mechi hata zile ngumu ambazo wengi waliamini wataangukia pua.

Wameifunga Coastal Union moja kati ya timu inayowasumbua sana, Azam FC na hata Namungo ambayo Yanga wamekuwa hawapati matokeo lakini safari hii wameondoka na alama tatu.

Simba SC imekuwa ikipata sare michezo mingi huku ikipoteza miwili na hivyo kukikofanya kikosi hiko kuwa nafasi ya pili nyuma ya Yanga kwa alama 13 ambapo inalazimika kuwaombea mabaya watani wapoteze zaidi yaa mechi nne huku wao wakiwa wanaondoka na point tatu kila mchezo.

Mbali na yote CV ya kocha, Pablo Franco Martin haioneshi kuwa anauzoefu wa kutosha na Soka la Afrika jambo ambalo litauwia ugumu Simba kutimiza malengo yao ya Michuano ya Afrika siku za usoni kama wataendelea kusalia  na Mhispania huyo.

Kwa sababu hizo kocha Pablo Franco nafasi ya kubakia Simba SC kwa misimu mingine ni sawa na Ngamia kupenya katika tundu la sindao.

Imeandikwa na @fumo255

Related Articles

Back to top button