Michezo

Simba inapaswa kushushwa Daraja – Mwakalebela

Mdau wa michezo na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (@Tanfootball), Frederick Mwakalebela, ameibua mjadala mzito kuhusu sakata la kutofanyika kwa mchezo wa watani wa jadi, Yanga na Simba mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Bongo FM, Mwakalebela amesema hakuna kigezo cha kutopeleka timu uwanjani kwa sababu ya kutopewa ruhusa ya kufanya mazoezi.

Kwa mujibu wa Mwakalebela, Yanga wanapaswa kupewa pointi zote tatu, huku Simba wakistahili kupigwa faini na kushushwa daraja kwa kushindwa kupeleka timu uwanjani.

Hata hivyo, amedai kuwa hatua hiyo haitatekelezwa kwa sababu amewahi kuwa ndani ya mfumo wa soka nchini na anaelewa namna maamuzi yanavyofanyika.

“Kitu kitakachotokea ni kwamba utasikia Simba, Yanga, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wameitwa na serikali. Kisha utasikia meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa amesimamishwa,” alisema.

Ameongeza kwa kusema kuwa hatimaye wadau hao wa soka watakaa pamoja kwa mazungumzo na kupanga tarehe mpya ya mchezo huo, hali inayoashiria kuwa kanuni za soka hazitafuatwa ipasavyo.

Mwakalebela amesisitiza kuwa kama angekuwa kiongozi wa Yanga, naye asingepeleka timu uwanjani kwa sababu kwa mujibu wa kanuni, Simba walistahili adhabu kali.

Sakata hili linaendelea kuzua mjadala mzito miongoni mwa wadau wa soka, huku wengi wakisubiri uamuzi wa mamlaka husika kuhusu hatima ya mechi hiyo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents