Michezo

Simba yajiandaa Morocco kimkakati

JUMAMOSI, wiki hii, macho na masikio ya mashabiki wa soka barani Afrika yatakuwa kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF kati ya wenyeji RS Berkane ya Morocco  na SIMBA SC  . Ni fursa ya kihistoria kwa SIMBA SC kuandika ukurasa mpya katika ramani ya soka la Afrika, lakini ili hilo litimie, kunahitajika maandalizi ya kina, mbinu sahihi na nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja. .
Simba klabu namba 4 kwa Ubora Afrika inapaswa kuelewa kuwa inapokwenda kucheza dhidi ya mabingwa wa Morocco RS Berkane, haikabiliani na kikosi kilicho na wachezaji tu, bali pia mfumo mpana wa watu wa nje ya mchezo wanaofuatilia mwenendo wa wapinzani wao kwa karibu. .
Ni wazi kabisa kuwa timu za kiwango hiki huwa na mashushushu na watu wa kiufundi wanaosaka taarifa muhimu zinazoweza kubadili matokeo ya mechi. Hivyo, Simba lazima iwe makini katika kila hatua, kuanzia mazoezini hadi wakati wa maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo. .
Ni wakati wa viongozi wa Simba, kuanzia benchi la ufundi hadi Kamati ya Utendaji kuhakikisha kila jambo linasimamiwa kwa umakini wa hali ya juu. Hakuna sababu ya taarifa za mbinu, kikosi au mikakati ya mchezo kuwafikia wapinzani kabla ya muda. Usiri mkubwa unahitajika kwani mara nyingi taarifa ndogo tu kuhusu hali ya mchezaji, aina ya mazoezi au mpango wa mbinu za mchezo zinaweza kuwa silaha kwa wapinzani. . Vilevile wachezaji wanapaswa kulindwa na kufuatiliwa kwa karibu katika kipindi hiki nyeti. Hii siyo tu kuhusu afya zao, bali pia mienendo yao ya kisaikolojia na kimwili. Ni wakati wa kuwakinga dhidi ya majaribu ya nje na kuhakikisha akili zao zinabakia kuuwazia mchezo pekee.
Ni muhimu kwa uongozi wa Simba kuwapa wachezaji utulivu, hamasa na mazingira bora ya maandalizi bila bughudha yoyote inayoweza kuathiri morali ya kikosi (Hapa hata machawa wasipewe nafasi ya kuwasogelea wachezaji)  .
Ni muhimu kwa Simba kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu, kujihami kwa umakini na pia kutumia nafasi chache zitakazopatikana kwa ufasaha. Mechi kama hizi huamuliwa na makosa madogo, hivyo kila mchezaji anatakiwa kuwa makini kwa asilimia 100 dakika zote 90. . Kwa ujumla, Simba inapaswa kwenda Morocco ikiwa timu moja yenye mshikamano, usiri mkubwa, maandalizi sahihi na mikakati madhubuti ya kiufundi na kisaikolojia.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents