Simbachawene aitaka bodi mpya kuiwezesha Taasisi ya Uongozi kuwa sura ya Afrika katika kuwajengea uwezo viongozi
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameiagiza bodi mpya ya Taasisi ya Uongozi kuhakikisha inatimiza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya taasisi hiyo kupata sura ya bara la Afrika katika kujenga uwezo wa viongozi wake.
Simbachawene alitoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua bodi mpya ya tano ya taasisi hiyo ambapo alisema ni muhimu bodi hiyo kuhakikisha inatengeneza taasisi imara na yenye fikra za mbele zinayotekeleza majukumu yake.
Alisema moja ya sababu kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kujenga uwezo wa viongozi wa bara la Afrika kuwa na mipango na mawazo endelevu ya maendeleo katika bara la Afrika hasa katika kutunza rasilimali na kukuza uongozi wa bara hilo.
Simbachawene alisema kuwa Taasisi ya Uongozi imejijengea umaarufu kama taasisi ya kikanda inayolenga kuimarisha uwezo wa viongozi wa Afrika katika kusimamia maendeleo endelevu.
Aliongeza kuwa taasisi kama hiyo inahitaji wajumbe wa bodi yenye umaarufu wa kimataifa na uelewa mpana na kuongeza kuwa uteuzi wao unapaswa kutegemea sifa binafsi na uzoefu unaohitajika kusaidia malengo ya taasisi.
”Nmezindua bodi mpya ya Taasisi ya Uongozi ambayo ni taasisi ya Kikanda na taasisi ya barani Afrika, bodi hii imeteuliwa na Rais kwa mujibu wa sheria, Rais amewateua na amewapongeza sana kwakupata nafasi hii. wajumbe wapya wa bodi wanakidhi vigezo vyote, Rais amewaamini katika nyadhifa hizi ili kuendeleza ukuaji wa bara hili. Tafadhali pokeeni uteuzi huu kwa heshima,” alisema Simbachawene
Kwa Upande wake Mwenyekiti Mpya wa Bodi hiyo ambaye ameingia kipindi cha pili kuongoza, Balozi Ombeni Sefue alithibitisha uwezo wa taasisi hiyo katika kukuza viongozi kote Afrika ili kushughulikia masuala muhimu yanayoathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya bara hilo.
Alisema kuwa mkazo wa Taasisi ya Uongozi katika maendeleo ya kiuchumi na maamuzi umechangia miradi muhimu kama vile ujenzi wa Reli ya Kisasa ya mwendokasi (SGR) na kukuza myororo wa thamani wa uongozi na kwamba taasisi hiyo imeendelea kuimarisha uwezo wa mawaziri, viongozi wa sekta binafsi,wakuu wa mikoa na wilaya.
“Tunaendelea kuhakikisha kuwa Taasisi inatimiza lengo lake la kuimarisha viongozi katika ngazi za kitaifa na kikanda,” alisema Balozi Sefue
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo, alielezea mafanikio kadhaa ikiwemo kuanzishwa kwa programu ya uongozi wa wanawake na kuthibitisha kuwa taasisi hiyo iko katika hali nzuri kifedha na inapata mchango mkubwa kutoka kwa vyanzo mbalimbali vinavyosaidia juhudi zake.
Singo alisema kuwa uongozi na wafanyakazi wa Taasisi ya Uongozi wameonesha kujitolea bila kuchoka, jambo ambalo limechangia mafanikio mbalimbali katika taasisi hiyo.
Bodi mpya ya wakurugenzi inayoongozwa na Balozi Ombeni Sefue, ina wajumbe wakiwemo Balozi Theresa Zitting (Balozi wa Finland nchini Tanzania), Dkt. Laura Torvinen, Balozi wa zamani wa Finland nchini Tanzania na Dkt. Brian Cawley, Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Taasisi ya Utawala wa Umma.
Wengine ni Balozi, Meja Jenerali (mstaafu) Gaudence Millanzi, Begun Taj, Balozi wa zamani wa Tanzania, Prof. Samwel Wangwe, mstaafu Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Dkt. Hamis Mwinyimvua, Mhadhiri Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Written by Janeth Jovin