Habari

Simbachawene amgeukia bosi NIDA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh.George Simbachawene, amemtaka Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kujitathmini yeye mwenyewe binafsi na kuona kama anastahili kuendelea kushika wadhifa huo ama la.

Kauli hiyo ameitoa akiwa mkoani Iringa, amemuagiza  Mkurugenzi huyo ajitathimini kuhusu suala la vitambulisho na  kama anaona hawezi basi amwambie Rais Samia Suluhu Hassan,  ameshindwa kazi hiyo ili nafasi hiyo ichukuliwe na mtu mwingine.

Waziri Simbachawene amesema tangu ameanza kupiga kelele kuhusu vitambulisho vya NIDA hadi sasa vilivyozalishwa ni milioni 2 tu na kusema hali hiyo hawezi kuivumilia, na kumuambia Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Dkt. Anold Kihaule, kama kazi imemshinda aseme ili apewe anayeweza kutimiza majukumu.

“Kwahiyo tangu nimeingia kwenye nafasi hii ya Uwaziri, kelele zote nilizopiga kwenye vitambulisho zimezalisha vitambulisho milioni 2 tu, na mimi siwezi kukubali ninachomwambia huyo Mkurugenzi Mkuu kama hii kazi imemshinda apewe kazi nyingine na hii aachie watu wengine, sawa ni mteule wa Rais, kama imemshinda amwambie,” amesema Waziri Simbachawene.

By-BAKARI WAZIRI

Related Articles

Back to top button