Singo: Tunatarajia watanzania wengi watakisoma kitabu cha Sokoine
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo amesema anatarajia watanzania wengi watakisoma kitabu hicho cha maisha na Uongozi wa Waziri huyo Mkuu wa zamani Edward Moringe Sokoine kwa kuwa kimeandika kwa lugha ya kiswahili.
Singo ameyyaxema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu cha maisha na uongozi wa Sokoine kilichoandikwa na taasisi hiyo ya Uongozi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).
Amesema kitabu hicho kimeandikwa kwa lugha ya kiswahili na walifanya hivyo ili kuungana na serikali katika kuendelea kukuza lugha hiyo na kwamba wanatarajia watu watajitokeza kwa wingi kukisoma.
Hata hivyo Singo amesema wakati wa mchakato na kuandika kitabu hicho walikumbana changamoto kadhaa ambazo hatoweza kuzisahau na kwamba zitabaki kuwa kumbukumbu kwake.
Amesema moja ya changamoto hiyo ni alimuomba Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Uongozi apeleke taarifa kwa Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango kuwa hawana fedha za kufanya jambo hilo na kiongozi huyo aliposikia hayo aliahidi kuzungumza na Rais na baada ya wiki mbili fedha zilipatikana.
“Tulikumbana na hali ya kipekee wakati tunaelekea kwa Dk Mpango na tulipotea njia jambo ambalo lilitufanya tukaingia ofisi tusiyotarajia, tukajikuta tupo mbele ya Rais Samia bila kutarajia huku tukiwa tumemsubirisha Makamu wa Rais kwa saa mbili, ila mama Samia alitusaidia kumpigia Dk. Mpango na kumweleza kuwa ametuchelewesha yeye, “ amesema Singo
Aidha aMEsema changamoto nyingine ambayo hataisahau wakati wa mchakato wa kuandika kitabu hicho ni kupigiwa simu usiku wa saa nne na Dk. Mpango ambaye alikuwa akiwakemea kwa kuchelewesha kitabu hicho na kuwaeleza hayuko tayari kuendelea kufanya kazi nao.
“Simu ile ilinishtua sana lakini maneno yake Dk. Mpango yalitufanya tuweke juhudi kubwa zaidi tukagawana kazi kwa kukisoma kitabu usiku kucha ili kuweza kukikamilisha,” alisema Singo
Kwa upande wake mtoto wa Sokoine ambaye pia ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Joseph Sokoine alisema kitabu hicho kimeandikwa wakati aliopanga Mungu na kwamba anamshukuru Rais Samia kwa kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.
“Pamoja na kwamba ni miaka mingi imepita na wengi ambao wangeweza kueleza mengi ambayo yangeweza kukipa kitabu hiki hazina kubwa zaidi ya historia, hawapo nasi tena naamini kama ambavyo rafiki yangu mmoja anavyopenda kunikumbusha kuwa kila jambo linatokea kwa wakati aliopanga Mungu, hivyo kitabu hiki kimeandikwa wakati aliopanga Mungu, tunamshukuru Rais kwa kulifanikisha hili,” alisema Balozi Sokoine
Written by Janeth Jovin