
Serikali ya Slovenia imeweka marufuku ya kusafiri dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, hatua iliyotangazwa rasmi siku ya Alhamisi kupitia taarifa ya serikali.
Hii inafuatia msimamo wa nchi hiyo kuhusu mzozo wa Palestina, ikiwa ni pamoja na kuitambua rasmi Palestina mwaka jana na kupiga marufuku mawaziri wawili wa mrengo mkali wa kulia wa Israel mwezi Julai.
Katibu wa Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje, Neva Grašič, alisema kupitia akaunti rasmi ya serikali katika mtandao wa X: “Kwa hatua hii, Slovenia inathibitisha dhamira yake kwa sheria za kimataifa, maadili ya msingi ya haki za binadamu, na sera ya nje yenye misimamo thabiti na ya kanuni.”
Slovenia, ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya, tayari imechukua hatua kadhaa dhidi ya Israel.
Mwezi Agosti, iliweka vikwazo vya silaha na kupiga marufuku uagizaji wa bidhaa kutoka maeneo ya Palestina yanayokaliwa na Israel kinyume cha sheria za kimataifa.
Aidha, ilipitisha msaada wa ziada kwa watu wa Gaza.
Kuhusu Netanyahu, Grašič alisema kuwa serikali imechukua hatua hiyo kwa sababu anashutumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa kutenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu huko Gaza.
“Umma unafahamu kuwa kuna mashauri yanayoendelea dhidi yake kwa tuhuma hizo,” aliongeza. “Kwa uamuzi huu, serikali inatuma ujumbe wazi kwa Israel: Slovenia inatarajia utii wa kweli wa maamuzi ya mahakama za kimataifa na sheria ya kimataifa ya kibinadamu.”
Slovenia imekuwa miongoni mwa mataifa ya Ulaya yaliyo mstari wa mbele kutaka kusitishwa kwa mapigano Gaza na kuongezwa kwa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Palestina.
Mwezi Julai, serikali hiyo ilitangaza marufuku ya kuuza, kununua na kupitisha silaha kwenda au kutoka Israel, wiki mbili tu baada ya kumtangaza Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, Itamar Ben-Gvir, na Waziri wa Fedha, Bezalel Smotrich, kuwa watu wasiotakiwa kuingia nchini humo, kutokana na matamshi yao ya “kuchochea mauaji ya halaiki” na vurugu dhidi ya Wapalestina.
Slovenia sasa inaendelea kuwa sauti yenye msimamo wa wazi katika kutetea haki za binadamu na sheria za kimataifa, hata inapokinzana na mataifa yenye nguvu duniani.





