Suala la miliki ubunifu siyo la muungano: BRELA
Na Janeth Jovin
MKURUGENZI wa Miliki Ubunifu kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Loy Mhando amesema kuwa suala la miliki ubunifu siyo jambo la Muungano kwani pande zote mbili yaani Tanzania bara na Zanzibar zimeweka sheria zinazosimamia katika kuratibu, kusimamia na kulinda haki za mbunifu.
Akizungumza mkoani Morogoro wakati akitoa wasilisho kuhusu umiliki ubunifu kwa waandishi wa habari waliopo kwenye mafunzo yanayotolewa na BRELA, Mhando amesema masuala ya umiliki Ubunifu siyo masuala ya Muungano kwani kila upande wa Muungano una taratibu tofauti wa kuratibu na kusimamia masuala ya umiliki ubunifu.
“Masuala ya miliki ubunifu si ya muungano kila pande ya Muungano kuna taratibu zake lakini tukienda kimataifa tunaenda kama nchi lakini tukirudi kila mtu anaenda kuyaweka katika utaratibu wao kulingana na mfumo wao wa kisheria”,amesema Loy.
Loy amesema kuwa miliki ubunifu imegawanyika katika makundi mawili ikiwemo ubunifu unaohusisha uzalishaji mali na utoaji huduma pamoja na hakimiliki na hakishiriki.
Amesema katika kulinda kazi za kibunifu nchini ili kuleta manufaa kwa mbunifu serikali imeweka mifumo ya sheria ambayo itasaidia kulinda kazi hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni na Majina ya Biashara BRELA, Lameck Nyangi akizungumza kuhusu ada za usajili wa kampuni mpya amesema ada zinalipwa kutokana na mtaji wa kampuni husika.
Aidha amesema sheria ya usajili wa kampuni katika kifungu cha nne mpaka cha tisa kimeeleza namna mkataba wa kampuni au kanuni za uendeshaji unatakiwa kuandaliwa.
Ameongeza kuwa usajili wa kampuni unafanywa kwa mujibu wa sheria ya kampuni ya Tanzania ya mwaka 2002 ambayo ilikuwa haina tofauti na sheria ya 1932 ambayo chimbuko lake ni sheria ya kiingereza ya mwaka 1929.
“Sheria ya mwaka 1932 ilifutwa na sheria ya mwaka 2002 kwa maana ilitengenezwa sheria mpya ya kampuni na hivyo kuwa na sheria mpya na ikabaki na sura ile ya 212 lakini sheria hii bahati mbaya ilipitishwa na Rais na kuanza kutumika mwaka 2006,kwa hiyo pamoja na sheria kutungwa katika kipindi cha miaka miaka sita iliendelea kutumika sheria ya mwaka 1932”,Amesema Nyangi
Written by Janeth Jovin