Bongo5 Makala

Super Sunday Makala: Dada pumzisha mwili wako, weupe sio mali

May 19, 2018 Kiongozi Mkuu wa kanisa la Anglikana nchini Uingereza Askofu Mkuu, Justin Welby alifungisha ndoa ya Mwanamfalme wa nchi hiyo, Prince Harry na mpenzi wake Meghan Markle. Harusi ya wawili hao ilihudhuriwa na wageni wengi maarufu duniani na kutazamwa na maelfu ya watu nchini humo na nje ya Uingereza.

Ndoa hiyo iliyofungwa katika kanisa la Kifalme la Mtakatifu George ndani ya kasri la Windsor, ilifanya siku hiyo kuwa bize kama daladala. Idadi kubwa ya watu walijikuta hawabandui macho katika runinga zao kuhakikisha hawapitwi na kile ambacho kilikuwa kinaendelea. Twende pole pole.

Lengo si kujadilli harusi hiyo bali muonekano wa Meghan Markle, alivalia shela jeupe lililotengenezwa na kampuni ya kifaransa iliyoko London, Givenchy.

Alikuwa ni mwenye kujiamini kiasi, tabasamu lake lilibeba furaha iliyokuwa imeujaza moyo wake, uso wake haukonekana kutaliwa na vitu vingi. Kitu hicho kilibubua mjadala kama sio utani hasa kwenye mitandao hapa nchini Tanzania, baadhi ya watu walidai kuwa Meghan Markle hapukapa make-up usoni mwake huko wengine wakieleza kuna namna uso wake uliwekwa tena kwa gharama kubwa zaidi.

Chanzo cha mjadala ni kutokana na harusi nyingi za sasa nchini bibi harusi uhudumia na timu ya warembeshaji. Hapa wengi hujikuta wakipoteza kabisa muonekano wao wa kawaida, wengi hutafuta kuonekana weupe hata kama asili yake haipo hivyo.

Hii ni kutokana weupe ni kitu ambacho uhusudiwa sana na baadhi ya watu wengi na kuamini mtu wa namna hiyo ndio mrembo. Ndiyo, ni kweli!, kuna makabila wanawake weupe hutolewa mahari kubwa zaidi ukilinganisha na wale ambao si weupe.

Vitu kama hivi na vinginevyo nyuma ya pazia vimepelekea kina dada wengi kuusaka weupe kwa gharama yoyote ile. Iwe kwa kutumia vipodozi vikali, vidoge na hata kemikali (mkorogo).

Msanii wa muziki wa Hip Hop nchini, Farid Kubanda ‘Fid Q’ katika wimbo wake uitwao Neno alioshirikiana na Isack Waziri Maputo ‘Lord Eyes’, alipata kusema; ‘Weupe ungekuwa mali ubuyu usingepakwa rangi,’.

Miaka kadhaa mbele msanii mwingine wa muziki huo, Nicas Marwa Machuche ‘Nikki Mbishi’ akatoa wimbo uitwao Dada Pumzisha Mwili Wako. Nyimbo zote hizi mbili zililenga kokomesha utamaduni wa kina dada kubadili rangi za ngozi zao na kuamini kuwa weupe utawafanya kuonekana wenye kuvutia zaidi.

Kwanini Weupe

Ukweli wa mambo ni kwamba mabinti/ kina dada wengi kwa sasa hawajiamini na muonekano wao wa asili, kujiamini kwao kumewekwa ndani ya vipodozi hatari na mambo mengine kama hayo. Nje hapo hakuna utulivu ndani ya nafsi zao, hata hivyo hakuja haja ya kuchanganyikiwa kote huko.

Dk. James P Comer anasema jinsi mtu anavyojiamini mwili ni sehemu ya anavyojiona kibinafsi, hilo laweza kuathiri kujiamiani kwa mtu na anavyofanya na asivyofanya maishani mwake.

Kitabu cha Questions Young People Ask & Answer That Work, kinatueleza kuwa kuna uvutano ambao umeenea sana kwenye runinga, vitabu na sinema. Wanaume na wanawake wengi wenye kuvutia wanakodolewa sana macho.

Kwa njia hiyo mawasiliano ya vyombo vya habari vingependa watu wasadiki kwamba maisha yapo hivyo, kitu ambacho sio sahihi. Kitabu hicho kinazidi kueleza mara nyingi vijana hushindwa kuelewa kwamba warembo wa magazetini na kwenye runinga uhudumiwa na timu ya kuwarembesha kabla ya kuonekana na watu wengine.

Wale wachache wanaosadiki kuwa maisha ndivyo yalivyo ndio uamua kutafuta muonekano mpya/weupe kwa gharama yoyote ila bila kujali muda mwingine waweza kuathiri hata afya zao. Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekuwa ikihakisha hilo halitokei lakini ukweli wa mambo wapo waliojikuta wakipata magonjwa hatari kama saratani ya ngozi kutokana na hilo.

Dunia ya sasa imetoa uhuru mkubwa wa watu kujiamulia mambo binafsi, lakini katika uhuru huu kuna hati hati kubwa ya kutumbukia katika mtego endapo uchaguzi utakuwa sio sahihi. Hii ina maana kuwa uhuru una mipaka yake na matakwa yake pia.

Waswahili wakasema maisha ni kama sahani iliyojaa kila aina ya uchafu, hivyo ni jukumu lako kutambua kipi kinakufaa katika sahani hiyo, hapo ndipo utaona ugumu wa uhuru kujiamulia na kuchagua mambo. Ukishindwa kujua hilo ndipo kuchanganyikiwa kunaanza, kila utakaloona katika vyombo vya habari na mitandao kuhusu urembo unasadiki kuwa ndivyo lilivyo kitu ambacho si kweli.

Twende Taratibu

Mkurugezi wa Career Development, Vicki L. Baum anasema wanawake wengi huvurugika akilini waendapo katika mahojiano ya kupata kazi, hufikiri ni kama kufanya matembezi na wapenzi wao. Muda mwingine huhisi kama wanatongozwa na matokeo yake hujikuta wakipoteza kazi ambazo walikuwa wakitazamia kuzipata.

Hata hivyo John T. Molly mtungaji wa kitabu cha Dress for Success anasema kuwa jinsi tunavyovaa huongeza sana maoni ya watu ambao tunakutana nao kila siku kitu ambacho kwa kiasi fulani huathiri jinsi wanavyotutendea. Weka nukta hapo.

Kamata maneno ya Vicki L. Baum; ‘wanawake wengi huvurugika akilini waendapo katika mahojiano ya kupata kazi,’. Mtu wa namna hii ni yule aliyekosa kujiamini kwa kile alichonacho au kuona kina upungufu fulani ndipo linakuja suala zima la vipodozi hatari na mavazi yasiyostahili katika eneo fulani.

Wanaochanganyikiwa si tu wale wanaokwenda katika mahojiano ya kazi bali hata Mwajuma Ndalambili wa Tandale kwa Mtogole hujikuta katika hali hiyo. Hadi kufikia hapo ni matokeo ya kutojiamini.

Ilipo Dawa

Kitabu kidogo cha Saikolojia kiitwacho Brighten Your Life kinatoa mbinu kadhaa kwa wale waliokosa kujiamini na muonekano wao na kuamua kujibadili. Naomba kunukuu kama kitabu hicho kilivyoeleza.

1. Tambua kuwa uwepo wako hapa dunia si kama ajali bali ni matokeo ya uumbaji wa Mwenyenzi Mungu na alikuwa na kusudi na kukuumba kama ulivyo na unavyooneka kwa sasa.

2. Kila wakati unapofanya kazi yoyote, fanya kama mafanikio ndiyo matokeo pekee yanayowezekana, watu wote wenye mafanikio hufanikiwa kwa mtazamo huu. Mtazamo huu utakuwezesha kutafakari juu ya kazi na nguvu iliyo ndani yako bila kujali muonekano wa nje, pia itapelekea ufanyie uchambuzi wa makini kabla ya kufanya kazi yoyote.

3. Epuka mchezo wa kujilinganisha na kushindana na wengine, kuendeleza tabia ya kushindana iwe pekee ndani yako kwa mambo unayofanya na si kwa wengine. Hivyo ni kujifunza kuweka malengo yako mwenyewe na kufanya kazi ili uyafikie.

Kujilinganisha na kushindana na wengine daima huwa ni mchezo usiofaa kwa sababu utajikuta ukitazama zaidi upungufu wako kuliko kile ulichonacho. Matokeo yake utatafuta namna ya kuziba upungufu huo na matokeo zaidi ya hapo, ndicho kimepelekea kuandika makala haya. Shukrani.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents