Habari

Taliban yaomba kuzungumza katika Mkutano Mkuu wa UN

Taliban wameomba kuhutubia viongozi wa ulimwengu katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wiki hii katika Jiji la New York. Waziri wa mambo ya nje wa kundi hilo alitoa ombi hilo kwa barua Jumatatu.

Kamati ya UN itatoa uamuzi juu ya ombi hilo. Taliban pia wamemteua msemaji wao wa Doha, Suhail Shaheen, kuwa balozi wa UN wa Afghanistan.

Kundi hilo ambalo lilichukua udhibiti wa Afghanistan mwezi uliopita, lilisema mjumbe wa serikali iliyong’olewa madarakani haiwakilisha tena nchi hiyo.

Ombi la kushiriki katika mjadala wa kiwango cha juu linazingatiwa na kamati ya utambulisho, ambayo wajumbe wake tisa ni pamoja na Marekani, China na Urusi, kulingana na msemaji wa UN.

Lakini wana uwezekano wa kukutana kabla ya kumalizika kwa kikao cha Mkutano Mkuu Jumatatu ijayo. Hadi wakati huo, chini ya sheria za UN, Ghulam Isaczai atabaki kuwa balozi wa Afghanistan katika shirika hilo la ulimwengu.

Anatarajiwa kutoa hotuba siku ya mwisho ya mkutano tarehe 27 Septemba. Hata hivyo, Taliban walisema ujumbe wake “hauwakilishi tena Afghanistan”. Pia, walisema kwamba nchi kadhaa hazimtambui tena Rais wa zamani Ashraf Ghani kama kiongozi.

Bwana Ghani aliondoka ghafla nchini Afghanistan wakati wanamgambo wa Taliban walipokuwa wakisonga mbele kuingia mji mkuu, Kabul, mnamo Agosti 15. Tangu wakati huo amekimbilia katika Falme za Kiarabu.

Wakati Taliban inadhibiti Afghanistan mara ya mwisho, kati ya mwaka 1996 na 2001, balozi wa serikali waliyoipindua alibaki kama mwakilishi wa UN, baada ya kamati ya utambulisho kuahirisha uamuzi wake juu ya madai ya kushinikiza kupata nafasi hiyo.

Katika mkutano wa UN Jumanne, Qatar iliwataka viongozi wa ulimwengu kuendelea kushirikiana na Taliban.

“Kuwasusia kutasababisha tu ubaguzi na athari zaidi, wakati mazungumzo yanaweza kuzaa matunda,” alisema mtawala wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani.

Qatar imekuwa kiungo muhimu nchini Afghanistan. Iliandaa mazungumzo kati ya Taliban na Marekani ambayo yalimalizika kwa makubaliano ya mwaka 2020 ya kuondoa vikosi vya Nato vinavyoongozwa na Marekani.

Bofya hapa chini kutazama.

https://www.instagram.com/p/CUHX7DyDiKg/

Credit by BBC.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents