Habari

TAMWA yatoa wito kwa wadau, serikali kushughulikia vikwazo vinavyowazuia watoto kupata elimu, kuingia shuleni

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimewataka wadau wa elimu, wazazi, walimu, viongozi, mashirika yasio ya kiserikali na maofisa wa serikali kushirikiana katika kushughulikia vikwazo vinavyowazuia watoto kuingia shuleni na kupata elimu bora.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Meneja wa Miradi na Mikakati TAMWA, Sylvia Daulinge wakati akizindua Makala inayoangazia umuhimu wa elimu bora na jumuishi kwa watoto walio hatarini kuacha shule iliyoandaliwa na chama hicho kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali la We World.

Daulinge ambaye ameyasema hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rode Reuben, amesema kila mtoto anastahili elimu bora, jumuishi na yenye usawa sio tu kuhusu mustakabali wao bali wa jamii nzima na kwamba kwa kuvunja vikwazo wanaweza kuunda fursa kwa watoto wote kustawi.

“Watoto wanaacha shule hasa katika maeneo yenye uhaba wa huduma inaotokana na umaskini, umbali mrefu wa shule, mila na desturi za jamii zetu pamoja na ukosefu wa rasilimali za kutosha za kumuwezesha mtoto kwenda shule. Watoto wenye ulemavu wanakumbwa zaidi na hali hii kwa sababu shule nyingi hazina miundombinu au rasilimali kukidhi mahitaji yao kielimu,” amesema

Amesema kwa hali hiyo ni lazima waendelee kuhamasisha na kushughulikia mizizi ya tatizo hilo la watoto kuacha shule kwa kuunda mazingira yanayowawezesha wanafunzi kubaki shuleni na kusaidia walio katika mazingira magumu hasa wasichana na watoto wenye ulemavu.

Meneja wa Miradi na Mikakati wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Sylvia Daulinge

Aidha amesema makala waliyoiandaa imeleta pamoja sauti za watoto, wazazi, walimu, mashirika na ofisa wa serikali ambao wamefunguka kuhusu jinsi ya kuvunja vikwazo vinavyowazuia watoto kupata elimu bora na sio bora elimu pamoja na kusisitiza haja ya haraka ya kukabiliana na changamoto kupitia uwezeshaji wa jamii, ushirikiano na kuboresha sera za elimu nchini.

“Makala hii inasisitiza haja ya sera na mikakati inayolenga kusaidia makundi hatarishi kama vile wasichana, watoto wenye ulemavu, watoto kutoka familia masikini na kutoka kwenye jamii zilizo pembezoni kwa kuboresha mazingira ya shule wanaweza kufanikisha elimu bora na watoto kufurahia kwenfa shule,” amesema

Daulinge amesema ushirikiano wa pamoja utasaidia kuhakikisha uwakilishi mzuri wa changamoto za kipekee zinazowakumba watoto katika mazingira mbalimbali na utofauti huo unatoa taswira ya kina nap ana ya hali ya elimu nchini ambayo itasaidia kubadilika kwa mazingira ya ufundishaji na uandikishwaji wa watoto kwa wakati ili kupata kizazi kinachopenda elimu.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents