
Tanzania imeripoti visa vya kwanza vya ugonjwa wa Mpox, wizara ya afya ilisema Jumatatu, ikiwa ni mara ya kwanza virusi hivyo kugunduliwa katika mlipuko uliokumba nchi kadhaa za Afrika.
Watu wawili ambao walikuwa na dalili za ugonjwa huo walitengwa na kupimwa Jumapili, waziri wa afya Jenista Mhagama alisema katika taarifa kwenye mtandao wa X.
“Kati ya washukiwa, mmoja ni dereva wa lori aliyesafiri kutoka nchi jirani hadi Dar es Salaam,” ilisema taarifa hiyo.
Ripoti ya kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika wiki iliyopita ilisema visa 6,034 vya mpox vimethibitishwa tangu mwezi Januari katika nchi 22, na watu 25 walifariki.
Mpox inaweza kuambukizwa kati ya wanadamu kupitia mawasiliano ya karibu ya kimwili. Inasababisha homa, misuli kuuma na vidonda vikubwa vya ngozi kama majipu, na inaweza kusababisha kifo.