TikTok yafungwa rasmi Marekani, Trump atairudisha??

TikTok imepigwa marufuku Marekani, Januari 19 baada ya mahakama ya juu zaidi nchini humo kupinga ombi lililowasilishwa na mmiliki wa mtandao huo ByteDance, kutaka marufuku hiyo ibatilishwe.
Mahakama hiyo imeamua kuwa sheria inayopiga marufuku mtandao huo wa kijamii haikiuki haki msingi za mtandao huo na watumiaji wake kama inavyodai Tiktok.
Rais mteule Donald Trump anayetarajiwa kuapishwa rasmi Januari 20 anasema, mustakabali wa Tiktok atauamua yeye.
TikTok imekabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya serikali duniani ikiwemo nchi kadhaa za Afrika.
Senegal na Somalia zimepiga marufuku mtandao huo wa kijamii huku kukiwepo maombi ya hatua kama hiyo kuidhinishwa katika nchi nyingine kama Kenya.
Sababu kubwa inayotolewa na walalamikaji binafsi na hata baadhi ya serikali za Afrika, ni hatari kwa usalama wa taifa pamoja na kudorora kwa maadili katika jamii wakitaka hatua ichukuliwe dhidi ya TikTok.
Mtandao huo umeshutumiwa kutumika kusambaza propaganda, kutumika kama chombo cha kuendeleza ulaghai lakini pia kusambaza maudhui yasiyo na staha.
Kenya ni miongoni mwa nchi zenye matumizi makubwa ya TikTok duniani ikiwa na 54% ya matumizi jumla na 29% ya watu wakiutumia mtandao huo kupata taarifa za habari.
Haya ni kwa mujibu wa ripoti ya kidijitali ya 2023 ya taasisi ya Reuters. Misri ina watumiaji milioni 33 na Nigeria wateja milioni 28.
Mnamo Agosti, bunge nchini Kenya liliafiki kutopiga marufuku TikTok kufuatia ombi la mlalamikaji, raia nchini humo aliyetaka mtandao huo upigwe marufuku.
Badala yake serikali ilikubali kuzingatia udhibiti wa maudhui. Katika kikao kati ya rais William Ruto, mkurugenzi mkuu mtendaji wa TikTok Shou Zi Chew alikubali kufungua ofisi nchini Kenya kuwajibika kusimamia ipasavyo maudhui yanayochapishwa.




