HabariMichezo

Timu ya wanawake ya Afghanistan imeruhusiwa kucheza na FIFA

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limetangaza kuwa timu ya wanawake wakimbizi kutoka Afghanistan itashiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano ya kirafiki ya kimataifa yatakayofanyika mjini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kuanzia Oktoba 23 hadi 29, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa ya FIFA, mashindano hayo ya kihistoria yajulikanayo kama “FIFA United” yatazikutanisha timu nne za wanawake: Afghanistan (wakimbizi), Chad, Libya na timu ya taifa ya UAE.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino, amesema kuwa hatua hii inaonesha dhamira ya FIFA katika kuhakikisha wanawake na wasichana kote duniani wanapata haki ya kushiriki michezo, kutimiza ndoto zao za soka, na kuendeleza vipaji vyao kupitia michezo.

“Zaidi ya kuwa mashindano ya kirafiki, mechi hizi ni alama ya matumaini kwa wanawake duniani kote,” alisema Infantino.

Kwa upande wake, timu ya taifa ya wanawake ya Afghanistan imethibitisha taarifa hiyo kupitia tovuti yao rasmi na kuandika: “Kutoka uhamishoni, wachezaji wetu watashiriki mechi yao ya kwanza ya kirafiki ya kimataifa chini ya FIFA, kama ‘Timu ya Wanawake Wakimbizi wa Afghanistan’.”

Timu hiyo imetaja ushiriki huu kama “hatua muhimu kuelekea kutambuliwa rasmi”, hasa baada ya miaka ya kunyimwa nafasi ya kushiriki michezo tangu Taliban waliporejea madarakani mnamo 2021.

Mnamo Mei 2025, FIFA ilitoa ruhusa ya kuundwa rasmi kwa timu ya wanawake wa Afghanistan walioko uhamishoni, na kumteua Pauline Hamel, mwenye umri wa miaka 53, kuwa kocha mkuu wa timu hiyo.

Bi Hamel alielezea furaha yake akisema: “Tumepata fursa ya kufanya kazi nao na sasa tutaangalia kwa karibu maendeleo yao.”

Tangu kuingia kwa serikali ya Taliban, wanawake nchini Afghanistan wamezuiwa kushiriki michezo, elimu, ajira na shughuli nyingi za kijamii.

Hata hivyo, kupitia uhamishoni, timu hii sasa inapigania haki ya kushiriki mashindano ya kimataifa, ikiwemo Kombe la Dunia, na imetoa wito kwa wachezaji wa kike kote duniani kuunga mkono juhudi zao.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents