
Wiki sita baada ya kuingia madarakani, Donald Trump amekwenda katika Bunge la Marekani linalodhibitiwa na Chama chake cha Republican kuhutubia.
“Tumefanya mambo mengi ndani ya siku 43 kuliko yaliyofanywa na tawala nyingi katika miaka minne au miaka minane, na ndio tunaanza,” alisema katika mkutano wa mabaraza yote mawili.
Trump amejigamba kuwa, “wengi” wanaamini ndiye rais mwenye mafanikio zaidi katika siku zake za mwanzo katika historia ya Marekani. Amejilinganisha na George Washington, na akajigamba kuhusu ukubwa wa ushindi wake katika uchaguzi.
Ameelezea orodha ndefu ya mafanikio – mamia ya maagizo, kusitishwa kwa misaada ya kigeni, viwango vya chini vya wahamiaji haramu, na kujiondoa katika mashirika na makubaliano ya kimataifa.
Pia alizungumza kwa kirefu kuhusu marufuku yake kwa wana michezo waliobadili jinsia katika michezo ya wanawake na hatua za kuifuta “itikadi ya woke” katika shule na jeshi la Marekani.
Wakati huo huo, wanachama wa Democratics – walikaa kimya kimya, huku rais akiwalaumu mara kwa mara kwa matatizo yote ya taifa hilo na Rais wa zamani Joe Biden na kuwaita “vichaa wa mrengo wa kushoto.”
Wengine walijibu kwa kushikilia mabango madogo yenye maneno kama “uongo” na “si kweli.”