Habari

Trump akana mashtaka 34 mahakamani, aweka rekodi

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amekana mashtaka 34 dhidi yake kwenye Mahakama ya New York, katika tukio ambalo lilikuwa la Kihistoria kwani amekuwa rais wa kwanza wa zamani wa Taifa hilo kufunguliwa mashtaka ya jinai.

Trump mwenye umri wa miaka 76, amefikishwa mahakamani jana siku ya Jumanne April 4, kwa mashtaka ya kumlipa mwanamke mmoja nyota wa filamu za ngono kabla uchaguzi, ili asizungumzie uhusiano wa kingono waliokua nao. Trump amewakosoa waendesha mashtaka nchini humo akisema  “wameitusi nchi hiyo.”

Muda mfupi baada ya kuwasili huko Mar-a-Lago, Florida, baada ya kurudi kutoka New York alikokanusha mashtaka ya jinai dhidi yake, Trump aliuhutubia umati wa wafadhili, marafiki zake wa kisiasa na wafuasi wake akisema hakudhani kwamba kitu kama yeye kufunguliwa mashtaka, ni jambo ambalo lingewahi kutokea nchini Marekani.

Trump amejitetea akisema hajafanya kosa lolote na kwamba mashtaka dhidi yake yanastahili kuondolewa mara moja. Anadai kuwa kosa lake kubwa lilikuwa kuitetea Marekani kutoka kwa wale wanaonuia kuiharibu.

“Kuanzia mwanzo Wademocrat walikuwa wanachunguza kampeni yangu, mnakumbuka? Walinishambulia kwa kufanya uchunguzi wa uongo, Urusi, Urusi, Urusi, Ukraine Ukraine, Ukraine, uongo wa kwanza wa kuniondo madarakani, uongo wa pili wa kuniondoa madarakani, uvamizi wa makaazi yake ya Mar-a-lago hapa,” alisema Trump.

Rais huyo wa zamani ambaye anapigiwa upatu kuipeperusha bendera ya chama cha Republican katika kuwania urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2024 amesema waendesha mashtaka kote nchini humo wanatumia kila mbinu ili wampate na hatia.

Imeandikwa na @fumo255

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents