Habari

TTCL yaingiza faida ya Bilioni 22.9, yazindua kituo cha kisasa FTTX Kijitonyama

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),David Nchimbi amesema Shirika la TTCL limeendelea na mkakati wa Mabadiliko ya kujiendesha Kibiashara ikiwa pamoja na kutengeneza faida ya sh. bilioni 22.9 (kabla ya kodi) katika mwaka wa fedha 2024/25.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo  wakati wa Uzinduzi wa Kituo cha Kisasa cha Kijitonyama FTTX Experience Center, alisema mafanikio hayo ya kutengeneza faida yanawapa wajibu wa kuhakikisha wanaendelea kuongeza mapato na kudumisha faida endelevu kupitia ufanisi, ubunifu na usimamizi madhubuti wa rasilimali za Shirika lao la TTCL.

Alisema awali Serikali iliwapa majukumu ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma za
mawasiliano nchini, sambamba na kujiendesha wao wenyewe kwa misingi ya kibiashara ili kuongeza ufanisi, mapato na uendelevu wa Shirika.

”Niwashukuru Kampuni ya Huawei na Kampuni ya Hisense kwa kushirikiana pamoja na TTCL katika mradi huu wa FTTX EXPERIENCE CENTER. Huu ndio ushirikiano tunaotaka kuuona ili kuchochea maendeleo ya teknolojia, ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa wananchi,”alisema

Alisema uzinduzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa Mkakati wa Kibiashara wa Shirika,hususan mradi wa FTTX pamoja na miradi mingine ya maendeleo ya miundombinu ya mawasiliano katika kuendeleza mageuzi ya kidijitali nchini.

”Ni kweli usiopingika Kijitonyama FTTx Experience Center ni kituo bora na cha kipekee kitakachotoa uzoefu pamoja na elimu kuhusu matumizi ya teknolojia za kidijitali.Kupitia kituo hiki,wananchi wataweza kujionea kwa vitendo namna ambavyo intaneti ya TTCL inavyoweza kubadilisha nyumba,Ofisi au Biashara kuwa za kidijitali na zenye ufanisi zaidi.

”Kituo hiki pia kitakuwa jukwaa la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa nyumbani,mifumo ya Ofisi za kidijitali na suluhisho za biashara mtandao,”alisema

Alisema kituo hicho kitasaidia kuongeza uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa TEHAMA katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.”Ni dhahiri kuwa maisha ya sasa yanahitaji intaneti yenye kasi na uhakika, inayowezesha na kurahisisha shughuli mbalimbali za kila siku—ikiwemo elimu mtandao, biashara
mtandao, huduma za kifedha na mawasiliano ya haraka na yenye tija,”alisema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu TTCL, Moremi Marwa alisema Shirika lao linatekeleza Mpango mkakati wa kibiashara wa miaka 10,ambao utekelezaji wake umeanza katika mwaka wa fedha 2025/26, mpango wenye lengo la kuleta mageuzi makubwa ndani ya shirika,hususan katika kuimarisha uwajibikaji, kuongeza uzalishaji wenye tija, na kuhakikisha uendelevu wa shughuli zao.

”Katika mageuzi haya yanayoendelea, mojawapo ya hatua muhimu ni utekelezaji wa mradi wa Faiba – Fiber To The X (FTTx). Mradi huu unalenga kusambaza huduma ya intaneti yenye kasi,uhakika na bora katika makazi, ofisi, na maeneo ya biashara.

”Shirika limekuja na Kijitonyama FTTX Experience Center,ni kituo cha kisasa ambacho kinaonesha mwendelezo wa ubunifu na mageuzi ya Shirika katika utoaji wa huduma za intaneti nchini.Kituo hiki ni cha mfano kinachoonesha dhamira ya Shirika katika kuboresha uzoefu wa wateja, kuelimisha matumizi ya teknolojia ya kisasa ya mawasiliano, na kuonesha uwezo wa huduma za Faiba (FTTX) katika kuleta mabadiliko ya kidijitali na maendeleo ya kiuchumi nchini,”alisema

Marwa alisema mteja akiwa katika kituo hicho, anaweza kuona matumizi ya kidigitali kwenye Smart Home, uwekaji wa huduma ya intaneti ya Faiba nyumbani ikisambazwa hadi katika vyumba mbalimbali, pamoja na maeneo ya ofisi na pia mteja ataweza kujionea teknolojia inayotumika katika utoaji wa huduma hizi za kisasa, jambo linaloonesha kwa vitendo namna huduma za Faiba zinavyofanya kazi na kuleta ufanisi katika mawasiliano.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents