Afya

Uganda imesitisha safari za ndege kutoka India baada ya kirusi cha Corona cha India kuripotiwa nchini humo (+ Video)

Uganda imepiga marufuku safari zote za ndege kutoka India kuanzia saa sita usiku tarehe 1 mwezi Mei ili kuzuia wimbi jingine la janga la corona nchini humo . Waziri wa Afya nchini humo Ruth Aceng amesema serikali imechukua hatua mbali mbali ili kuzuia kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi hivyo .

Hakuna abiria kutoka India atakayeruhusiwa kuingia nchini humo bila kujali alikotokea na abiria wote waliopitia au kutoka India katika siku 14 zilziopita pia hawatakubaliwa kuingia nchini humo .

Wasafiri wote kutoka India wataaowasili Uganda kabla ya kuanza kutekelezwa kwa marufuku hiyo watatakiwa kuwa na cheti cha kuthibitisha kwamba wamepimwa na kupatikana bila virusi vya Corona katika kipindi cha saa 120 wakati sampuli zilipochukuliwa kutoka kwao.

Wizara ya Afya nchini Uganda imeongeza kwamba wote watakaowasili nchini humo kabla ya marufuku hiyo kuanza kutekelezwa watapimwa Corona pindi watakapowasili na watakaopatikana kuwa bila virusi hivyo watatakiwa kujitenga wenyewe na kisha kurejea kwa vipimo baada ya siku 5 hadi 10 .Watakaopatikana na Corona watalazimika kuwekwa chini ya karantini ya serikali ambayo watagharamia wenyewe

Hata hivyo kuna safari kutoka India ambazo hazitaathiriwa na marufuku hiyo na ni pamoja na ;

  • Safari za ndege za mizigo ambazo wahudumu wake hawataruhisiwa kutoka kwneye ndege zao
  • Kusimama kwa muda wa safari za ndege ambapo abiria hawashuki
  • Ndege ambazo zitapatawa na hali ya dharura
  • Operesheni zinazohusiana na misaada ya kibinadamu ,misaada ya matibabu na huduma za uokoaji zilizoidhinishwa na mamlaka husika
  • Raia wa Uganda wanaorejea nyumbani kutoka India kwa matibabu

Wasafiri kutoka Marekani , Uingereza, Falme za Kiarabu, Uturuki, Afrika Kusini, Ethiopia, Sudan Kusini na Tanzania wanapaswa kuzingatia kuahirisha safari zisizo za lazima kwenda Uganda.

Msafiri yeyote kutoka nchi zilizo hapo juu pamoja na raia wa Uganda atafanyiwa vipimo vya COVID-19 katika Sehemu za Kuingia ikiwa ni pamoja na Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Entebbe.

Watu katika Kitengo cha 2 na 3 ambao wamepokea chanjo yao kamili ya COVID-19 na hawana dalili wataruhusiwa kuingia nchini bila hitaji la upimaji wakati wa kuwasili.

 

Siku ya alhamisi Uganda ilitangaza kwamba mtu mmoja amepatikana na aina ya kirusi cha Corona cha India .Sampuli kutoka kwa mtu huyo aliyeambukizwa, ambaye anapata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa ya Mulago katika mji mkuu Kampala, ilichukuliwa tarehe 26 Machi.

Nchi hiyo pia imerekodi maambukizi ya aina ya virusi hivyo kutoka Uingereza, Afrika Kusini na Nigeria.

Kuthibitishwa kwa aina hiyo ya virusi kutoka India kunakuja wakati huu ambapo India inapambana na wimbi la pili la virusi hivyo ambalo limesababisha maafa ya maelfu ya watu na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaoambukizwa kila siku

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Virusi nchini Uganda, Dk Pontiano Kaleebu, alisema kuwa msisitizo zaidi utalazimika kuwekwa katika hatua za kuzuia na upimaji wa watu katika mipaka ya nchi hiyo.

Kampeni ya Chanjo

Waziri Aceng amesema kuanzia wiki ijayo kutakuwa na kampeni vijijini ,katika masoko na maeneo ya kuabudu kuwahamasisha watu kuhusu umuhimu wa kwenda kuchanjwa dhidi ya virusi vya Corona . Amewahimiza raia wa Uganda kufuata masharti na maelekezo yote yaliyotolewa na serikali ili kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo .

“Naziomba jamii na viongozi wa jamii kuwa waangalifu na kuwatambua kumtambua msafiri kutoka nchi ambazo zimetajw akatika orodha hii na kuripoti kwa mamlaka za wilaya’ amesema waziri huyo

Uganda ilianzisha awamu ya kwanza ya kampeni yake ya chanjo mnamo Machi baada ya kupokea dozi 864,000 za chanjo ya AstraZeneca kupitia mpango wa kimataifa wa Covax, na 100,000 zaidi kutoka India.

Watu 304,000 tu wamepewa dozi ya kwanza hadi sasa.

Awamu ya kwanza inawalenga wafanyakazi walio mstari wa mbele kupambana na virusi hiyo – pamoja na wale walio katika sekta ya afya na elimu, wazee na watu wazima walio na hali nzuri ya kiafya.

Nchi ilianza kupunguza masharti makali ya kupambana na janga hilo hatua baada ya nyingine mnamo Mei mwaka jana. Hatua za kuzuia maambukizi , kama vile kuvaa barakoa na kujitenga sasa zinapuuzwa na watu wengi.

Nchi nyingine zilizopiga marufuku ya safari za ndege India

Uamuzi wa Uganda kupiga marufuku safari za kutoka India unajiri siku mbili tu baada ya taifa jirani la Kenya pia kutangaza marufuku ya muda ya safari za ndege kutoka India ambayo imesakamwa na idadi ya juu ya maambukizi ya Corona .

Waziri wa Afya nchini humo Mutahi Kagwe alisema’ hali nchini India imekuwa mbaya sana…. Na kulazimu kuzuiwa kwa safari za ndege kwa siku 14 zijazo’

Nchi nyingine zilizopiga marufuku safari za ndege India ni pamoja na Canada, falme za kiarabu na Uingereza -marufuku zinazoanza kutekelezwa siku ya jumamosi lakini hazitathiri ndege za kubeba mizigo.

Katika marufuku ya Kenya ,abiria wanaoingia nchini humo katika kipindi cha 72 zijazo watatakiwa kuwekwa karantini kwa kipindi kifaacho.

Siku ya jumatano India ilivunja rekodi kwa kusajili maambukizi mapya 360,000 ya corona na zaidi ya vifo vya watu 3000 huku maambukizi yakizidi kuongezeka katika taifa hilo la watu bilioni 1.3.

Bofya hapa chini kutazama.

https://www.instagram.com/tv/COUnuIUB_lm/

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents