AfyaFahamu

Ujue kwa undani Ugonjwa wa MonkeyPox

Je, tunapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu Homa ya Nyani?

.

Chanzo cha picha,Reuters

Maelezo ya picha,Dawa yapakwa kwenye uso wa mtoto mwenye mpox
22 Agosti 2024

Kuenea kwa kasi kwa ugonjwa wa Homa ya nyani inayojulikana kama mpox – barani Afrika kumetangazwa kuwa dharura ya kimataifa.

Aina mpya ya virusi hivyo ndio kinachotia watu wasiwasi , lakini bado kuna maswali mengi ambayo hayajajibiwa.

Je, inaambukiza zaidi? Hatujui. Je, ni hatari kiasi gani? Hatuna data. Je, hili litakuwa janga?

“Lazima tuepuke mtego wa kufikiria kuwa hii itakuwa kama Covid na tutakuwa na vizuizi – au iwapo utachukuliwa kama mpox ilivyokuwa mwaka 2022,” anasema Dk Jake Dunning, mwanasayansi na daktari ambaye amewahi kutibu wagonjwa wa mpox nchini Uingereza.

Ili kutathmini tishio – licha ya kutokuwa na uhakika – kwanza tunahitaji kutambua huu sio mlipuko wa kwanza wa mpox, bali wa tatu.

Yote inatokea kwa wakati mmoja, lakini inaathiri vikundi tofauti vya watu wenye tabia tofauti.

Virusi hivi vinatajwa kulingana na “clade” – kimsingi tawi gani la aina ya familia virusi vya mpox vinatoka?.

  • Clade 1 au tawi la kwanza linasababisha maambukizi mengi magharibi na kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC). Huu ni mlipuko ambao umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya muongo mmoja. Huenezwa zaidi kwa kula wanyamapori walioambukizwa wanaojulikana kama nyamamwitu. Wale wanaougua wanaweza kueneza virusi kwa watu wanaowasiliana nao kwa karibu na watoto wengi huathirika .
  • Tawi la pili ni aina mpya ya familia ya mpox na inasababisha milipuko mashariki mwa DRC na nchi jirani. Aina hii inaenezwa kupitia barabara za malori huku madereva wakifanya mapenzi na jinsia tofauti mbali na wafanyabiashara wa ngono walioambukizwa, huku watu hao nao pia wakiwapitishia watoto kupitia mgusano wa karibu.
  • Tawi la tatu ni mlipuko wa mpox ambao ulienea kote duniani mwaka 2022 na ulikuwa na uhusiano mkubwa na ngono, wakati huu ukiwaathiri zaidi, wapenzi wa jinsi moja (98.6% wakiwa wanaume nchini Uingereza) na vile vile watu walio karibu nao. Mlipuko huu haujaisha.

Madereva wa malori na wafanyabiashara wa ngono

Shirika la Afya duniani WHO limesema aina ya kwanza ya virusi hivyo ni sababu kuu ya kutangaza Dharura ya Afya ya Umma ya Kimataifa.

Aina hii ya virusi imeenea katika nchi ambazo hapo awali zilikuwa hazijaathiriwa na mpox – Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda.

Viliripotiwa kwa mara ya kwanza mwaka huu, lakini uchambuzi wa vinasaba umeonesha kuwa kwa mara ya kwanza uligunduliwa mwezi Septemba 2023 katika jiji la uchimbaji dhahabu la Kamituga, Mkoa wa Kivu Kusini, DRC.

“Kuna biashara ya ngono katika jiji la migodi na imeenea kwa kasi hadi nchi za mpakani kwa sababu ya harakati kubwa za watu,” Leandre Murhula Masirika, mratibu wa utafiti wa idara ya afya, ananiambia kutoka Kivu Kusini.

Alisema kulipia ngono ndiyo sababu ya kuenea kwa virusi, lakini pia husambazwa kutoka kwa mzazi hadi kwa mtoto au kati ya watoto na pia uhusishwa na kuharibika kwa mimba.

Kuzuka kwa kirusi kipya cha aina ya Clade 1b kunaonekana tofauti kabisa na kile cha Clade 1a.

“Kweli ni tofauti kwa sababu upele ni mbaya zaidi, ugonjwa unaonekana kuendelea kwa muda mrefu, lakini zaidi unachangiwa na maambukizi ya ngono kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine na haujahusishwa na ulaji wa nyama ya porini,” Prof Trudi Lang, kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, aliniambia kwenye kipindi cha Inside Health cha Radio 4.

Aina hii mpya inaonekana tofauti, lakini bado hakuna ushahidi kamili kwamba mabadiliko hayo yamesababisha virusi hivyo kuambukiza zaidi.

Kuingia kwa wafanyabiashara wa ngono wanaogusana kimwili na watu wengine wengi pia kunaweza kuongeza mlipuko.

“Uambukizaji kupitia mitandao ya ngono hutokea kwa haraka zaidi, haimaanishi kwamba virusi vyenyewe vinaweza kuambukizwa zaidi,” kwa mujibu wa Dk Rosamund Lewis, kiongozi wa wa ugonjwa wa Mpox katika Shirika la Afya Duniani.

Virusi hivyo haviambukizwa kupitia zinaa bali huenezwa wakati watu wanapogusana kimwili, na ngono ni wazi inahusisha mgusano wa karibu.

.

Chanzo cha picha,Reuters

Maelezo ya picha,Mtoto wa miaka sita ambaye ni mwathiriwa wa Homa ya Nyani

Pia kuna kutokuwa na uhakika kuhusu jinsi mikurupuko ya sasa ilivyo hatari.

Sio vifo vyote vinavyorekodiwa kwani watu wengine wanatafuta usaidizi wa “kienyeji” badala ya dawa za hospitali. Na hatujui ni watu wangapi wanaambukizwa – ambao baadhi yao wanaweza kuwa na dalili ndogo au la.

“Hatujui idadi ya walioambukizwa na kwangu hiyo ni mojawapo ya mambo muhimu yasiyojulikana,” anasema Prof Lang.

Historia inasema kwamba milipuko ya Clade 1 ni hatari zaidi kuliko Clade 2. Katika milipuko ya awali hadi 10% ya watu waliougua ugonjwa wa Clade 1 walikufa.

Na viwango vya vifo havisababishwi tu na virusi hivyo. Utapiamlo, VVU visivyotibiwa vinavyoharibu mfumo wa kinga au kutopata huduma ya hospitali vyote vinaweza kuongeza kiwango cha vifo.

Shirika la Afya duniani linasema 3.6% ya wagonjwa wa homa ya nyani iliosababishwa na aina ya Clade 1a mwaka 2024 walifariki. Hatahivyo haina idadi sawa na aina ya virusi vipya vya Clade 1b.

Kama siku za mwanzo za VVU

Zaidi ya watu 500 tayari wamefariki katika mlipuko wa ugonjwa wa mpox katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mwaka huu.

Tishio lililowekwa kwa nchi na majirani zake liko wazi.

“Hatujaweza kudhibiti virusi hivi katika Kivu Kusini,” anasema Leandre Murhula Masirika.

“Tunahitaji uingiliaji kati wa haraka na mkubwa kudhibiti milipuko huu na kuuangamiza kabisa”

Prof Lang, ambaye anafanya kazi na timu nchini DRC, analinganisha na siku za mwanzo za VVU.

Ninapomuuliza kuhusu hili anasema ni msemo unaotumika “si mara nyingi sana na kwa hakika sio jambo dogo”.

Anasema: “Mchanganyiko wa vijana wanaofanya biashara ya ngono na waliodhulumiwa, familia, madereva pamoja na watoto walio karibu na haya yote ambao ndio waathiriwa wa kwanza wa mlipuko huu ni hali sawa kama ile ya siku za mwanzo za VVU, ambapo kwa kweli ilisambazwa sana na wafanyakazi wa malori.”

Tishio la kimataifa?

Homa ya Nyani haitarajiwi kuwa tukio la kiwango cha Covid. Tayari ni karibu mwaka mmoja tangu aina mpya ilipoibuka mwezi Septemba 2023.

Hali inayowezekana zaidi nchini Uingereza na nchi kama hizo ni mtu kurudi na virusi na kuwa mgonjwa.

Hii imetokea mara nyingi huko nyuma nchini Uingereza na taifa hilo linaendelea kuripoti kesi za mpox zilizohusishwa na milipuko ya 2022 ya virusi vya aina ya Clade 2.

Kesi hizi zilizoingia kutoka nje zinaweza kufikia mwisho wake au kuenea kidogo ndani ya makaazi kutokana na kugusana kimwili miongoni mwa watu.

Uswidi ilipata kesi ya kwanza ya Clade 1b nje ya Afrika, na hakuna usambazaji zaidi umeripotiwa.

Hali inayotia wasiwasi zaidi itakuwa mtoto mchanga aliyeambukizwa kuisambaza kwenye shule ya chekechea ambapo anacheza na watoto wengine na kusababisha mlipuko.

Hali hiyo ndio kile kinachozingatiwa kuwa kinaweza kutokea nchini Uingereza.

“Hapana, sidhani kama hii itakuwa kubwa,” Dk Jake Dunning alisema.

“Ninakerwa kidogo na kushtushwa na watu wanachozungumzia kuhusu kile kilichotokea mwaka 2022 na nikifikiria kuwa vivyo hivyo vitatokea tena.”

.

Chanzo cha picha,Reuters

Maelezo ya picha,Chanjo ya ndui pia inaweza kulinda dhidi ya mpox

Jibu litakuwa kutafuta watu ambao walikutana na mtu yeyote aliyeambukiza na kuwachanja, badala ya programu kubwa ya chanjo.

Itakuwa rahisi kukabiliana na kesi zozote zinazoingia nchini Uingereza kuliko katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambayo inakabiliwa na migogoro na changamoto za kibinadamu.

Bado hakuna chanjo maalum za Homa ya Nyani lakini chanjo ya ndui hufanya kazi dhidi ya ugonjwa huo.

Virusi vya ndui na tumbili ni virusi vya Orthopox na kinga kwa moja husababisha ulinzi kwa nyingine.

Kumalizika kwa kampeni za chanjo ya ndui – baada ya ugonjwa huo kutokomezwa mwaka wa 1979 – ni moja ya sababu ya mpox kuanza kusambaa.

Wale ambao walipata chanjo ya ndui wakiwa watoto, licha ya mfumo wa kinga uliozeeka, bado wanapaswa kuwa na ulinzi fulani.

Watu wenye hitaji kubwa la chanjo ndio kiini cha mlipuko huo barani Afrika.

Dk Dunning anasema: “Tunashangaza sana kushiriki zana za kuzuia mpox, haswa chanjo na hiyo haiwezi kukataliwa.

“lakini ni dhahiri kwangu kuwa ushindi mkubwa kwetu ni kudhibiti milipuko hii kwenye chanzo.”

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents