Habari

UN yataka uchunguzi mauaji ya wanafunzi Sudan

Umoja wa Mataifa umetaka kufanyike uchunguzi wa mauaji ya wanafunzi watano wakati wa maandamano ya raia nchini Sudan ya kushinikiza serikali ya kiraia kabla ya mazungumzo kuhusu serikali ya mpito nchini humo.

Unruhen im Sudan (Getty Images/A. Shazyl)

Kwa mujibu wa shirika la habari la DW, Taarifa iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetoa mwito kwa mamlaka kuchunguza na kuwatia hatiani watuhumiwa wa ukatili huo dhidi ya watoto na kuongeza kuwa hakuna mtoto atakayezikwa akiwa na sare za shule.

Wanafunzi waliouawa walikuwa wa kati ya miaka 15-17. Wakati UNICEF ikitoa mwito huo, kiongozi wa baraza la kijeshi nchini Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amelaani mashambulizi dhidi ya wanafunzi hao na kuyaita ni uhalifu usiokubalika, hii ikiwa ni kulingana na kituo cha televisheni cha serikali.

Amenukuliwa na kituo hicho alipozungumza na waandishi wa habari wa Sudan akisema kile kilichotokea Al-Obeid ni cha kusikitisha. Kuwaua raia walioandamana kwa amani ni uhalifu usiokubalika na wahalifu wanatakiwa kuwajibishwa mara moja.

Sudan Khartoum | Friedensgespräche (picture-alliance/AA/M. Hjaj)Waandamanaji wameendelea kushinikiza baraza la mpito la kijeshi kukabidhi madaraka kwa raia

Waandamanaji wanavituhumu vikosi vya jeshi vinavyoongozwa na jenerali mwenye mamlaka makubwa nchini humo Mohamed Hamdan Dagalo kwa mauaji hayo ya vijana watano, wakati wa maandamano hayo katika mji wa Al-Obeid siku ya Jumatatu.

Jana, katika mji mkuu wa Khartoum, mamia ya raia waliandamana kwenye mitaa miwili ya al-Riyadh na Burri kufuatia mauaji ya waandamanaji, pamoja na wanafunzi hao. Hassan Osman, mmoja wa waandamanaji hao aliliambia shirika la habari la AFP kwamba “Mahitaji yetu ni serikali ya kiraia kwa sababu itatoa haki kwa mashahidi hawa waliouawa. Kila siku watu wanauawa, tunataka chombo huru ama cha kimataifa kuchunguza kwa sababu hatuuamini mfumo wa mahakama. Kila siku watu wanakufa, kama huko al-Obeid

wanafunzi.. kwa sababu tu walikwenda kutoa hisia zao!!”

Ni mauaji yanayotokea wakati viongozi wa kiraia wakijiandaa kufanya mazunguzo na majenerali wa baraza la kijeshi hii leo ya kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa serikali ya kiraia, wiki mbili baada ya kutiliana saini makubaliano ya kugawana madaraka mapema mwezi huu.

Serikali ilitangaza amri ya kutotembea nyakati za usiku katika miji minne iliyopo jimbo la Kordofan Kaskazini kufuatia vifo hivyo, wakati makundi ya waandamanaji yakiitisha maandamano ya nchi nzima dhidi ya mauaji hayo. Shule zote za eneo hilo pia zimeamriwa kusitisha masomo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents