Urusi imeripotiwa kutuma hadi wanajeshi 200 nchini Equatorial Guinea kulinda kiti cha urais, huku ikiendelea kupanua uwepo wake barani Afrika.
Ripoti za vyombo vya habari zinasema kwamba Warusi wanafundisha wanajeshi waandamizi katika miji mikuu miwili ya nchi hiyo – mji mkuu Malabo na Bata.
Ripoti za wanajeshi wa Urusi waliotumwa nchini humo kwa mara ya kwanza ziliibuka mwezi Agosti.
Urusi, ambayo imekuwa ikitaka kupata ushawishi zaidi barani Afrika, katika miaka ya hivi karibuni imetuma maelfu ya mamluki Afrika Magharibi na Kati ili kulinda tawala za kijeshi na kuwasaidia kupambana na waasi.
Shirika la habari la Reuters lilinukuu vyanzo vikisema kwamba Warusi kati ya 100 na 200 walikadiriwa kufika katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Ilisema kuwa baadhi yao wana uwezekano wa kuwa sehemu ya Corps Africa, kikosi cha kijeshi kilichojulikana hapo awali kama Wagner kabla ya kubadilishwa jina na kuwa chini ya udhibiti wa kijeshi wa Urusi.
Siku ya Jumatano, Tutu Alicante, mwanaharakati wa haki za binadamu mwenye makao yake nchini Marekani kutoka Guinea ya Ikweta, aliliambia shirika la utangazaji la serikali ya Marekani VOA kwamba madai ya kuwepo kijeshi nchini humo yanaweza kudhoofisha maslahi ya kijiografia ya Marekani.
Alisema kuwa Urusi “bila shaka inaimarisha misuli yake ya kijeshi na kiuchumi” kupitia uwepo wa wanajeshi nchini humo.
Marekani katika siku za nyuma imekuwa na uwekezaji ikiwa ni pamoja na katika sekta ya nishati ya nchi lakini maslahi yamepungua.
Baadhi ya nchi za Afrika Magharibi ambazo zimekuwa na mapinduzi katika miaka ya hivi karibuni zimejitenga na washirika wa jadi wa Magharibi kama vile Ufaransa, zikizishutumu kwa kutofanya vya kutosha kukomesha uasi wa wanajihadi, huku zikitafuta uhusiano wa karibu na Urusi.