Utafiti wabaini bodaboda, wavuvi, migodini makundi mapya maambukizi ya Ukimwi

UTAFITI umeonesha kuwa kundi la bodaboda, jamii za wavuvi na kwenye migodi ni moja ya makundi mapya yaliyopo hatari kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na AVAC, Mchumi Mwandamizi na Kaimu Meneja sehemu ya Mipango na Bajeti TACAIDS, Renatus Mukasa amesema katika makundi hayo vijana ndio waathirika zaidi.
Amesema kwa wastani, maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi kwa wenye umri wa miaka 15 ni makubwa zaidi kwa wanawake kuliko wanaume hapa nchini na kwamba hali hiyo inaweza kuchangiwa na mwamko mdogo wa wanaume kupima maambukizi.

“Kwa mujibu wa utafiti huu wa mwaka 2022-2023 kuhusu maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi Tanzania umebaini makundi mengine maalum ambayo ni hatari kwa maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ni pamoja na kundi la bodaboda, Jamii za Wavuvi na jamii za kwenye Migodi na Madini.
“Haya ni Makundi maalumu ambayo yameongezeka kutoka kwenye makundi yale matano ambayo tafiti za awali zilibaini kuwa ni wanawake wanaofanya biashara ya ngono, wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao, watumiaji wa dawa za kulevya hususani wanaojidunga sindano, wasichana balehe na wanawake vijana wenye umri kuanzia miaka 15-24 pamoja na kundi la wanaume Vijana”. Amesema Mukasa
Aidha amesema katika kuendeleza afua za udhibiti wa VVU na UKIMWI hususani kwenye makundi hayo, Serikali imeandaa na inaendelea kutekeleza mpango mkakati wa udhibiti wa VVU na Ukimwi wa mwaka 2021 hadi 2026.
Amesema mpango mkakati huo umeonesha afua zinazotekelezwa kwa kila sekta binafsi na umma kuhusiana na kuandaa mipango na mikakati mbalimbali inayohusiana na utekelezaji wa afua kwa vijana na kwamba miongoni mwa program zinazotekelezwa ni pamoja na mradi wa timiza malengo.
“Mradi huu wa timiza malengo unatekelezwa kwa awamu ya tatu na unahusu wasichana balehe na wanawake vijana kuanzia umri wa miaka 15 hadi 24 na ulianza kwenye mikoa ya kipaombele mitano ambayo ni Dodoma, Singida, Tanga, Geita na Morogoro, hata hivyo tumeongeza mikoa ya Lindi, Ruvuma lengo ni kuhakikisha vijana wanafikiwa,” amesema
Amesema lengo kubwa la program hiyo ni kutekeleza zile afua zinalenga kubadili tabia kwa vijana ikiwemo kuandaa miongozo na mitaala ya elimu ya afya ya uzazi, stadi za maisha pamoja na udhibiti wa VVU na UKIMWI.
“Kupitia program hii tumeshirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Wizara ya Elimu na Tamisemi kuhakikisha kwamba mtaala wa elimu ya afya ya uzazi, ukatili wa kijinsia, stadi za maisha pamoja na UVV na Ukimwi unaingizwa kwenye mitaala ya elimu shule za msingi hadi vyuo vya elimu ya juu,” amesema na kuongeza
“Lengo tunataka kuanzia chini watoto wafundishwe namna ya kuzuia, kujilinda na maambukizi ya VVU, kwa miaka inayokuja itakuwa na faida kubwa katika kubadili tabia hasa za vijana balehe,” amesema
Written by Janeth Jovin