Vijana CCM wapewa ujasiri wa kugombea ubunge, udiwani

Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wilayani Songea mjini wamehimizwa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika baadae mwaka huu.
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Halmashauri ya Taifa, Hemed Chale wakati akiongea na vijana wa CCM wilayani Songea.
Chale, aliyeambatana na viongozi waandamizi wa CCM wa wilaya na pia wa Umoja wa Vijana (UVCCM),amewataka vijana kujiamini na kuthubutu kwa kujitokeza kuchukua fomu, iwapo wanaamini kuwa wanaweza.
“Vijana wenzangu niwaondoe hofu, msiwe na mashaka. Kijana lazima awe na uthubutu, lazima ujiamini…Ukifika muda; ukiona unaweza, unatosha; kachukue fomu,” alisema Chale.
Akisifu mchango wa vijana wa kiume na wa kike, Chale alisema, kundi hilo ndio injini ya Chama cha Mapinduzi na akasisitiza kuwa taifa la Tanzania limejengwa na linaendelea kujengwa na vijana.
“Sisi sote ni mashahidi. Kuna vijana wengi sana wapo kwenye nafasi za chama na Serikalini. Tuna mawaziri wengi ambao wanatokana na vijana na kazi zao nzuri zinaonekana,” alisisitiza akijenga hoja kuwashawishi vijana kujitokeza kugombea.
Naye Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Songea alisema, Mwinyi Msolomi, akiwahamasisha vijana wakagombee alisema hakuna mwenye jimbo au kata yake, bali kila mtu ana haki ya kuwania nafasi hizo.
“Utakapofika wakati, hakuna kata mwenye nayo, hakuna jimbo mwenye nalo, isipokuwa ngazi ya Rais tumemaliza kazi,” alisema Mwenyekiti huyo huku akishangiliwa na vijana.
Ikumbukwe kuwa CCM ilifanya mkutano wake mkuu maalumu Januari 18 na 19, 2025 ambao pamoja na mambo mengine ulimchagua uliwapitisha Rais Samia Suluhu Hassan na Dkt Hussein Mwinyi kuwa wagombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar.
Mkutano huo pia ulimpitisha Dkt Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa Rais Samia kufuatia ombi lililokubaliwa la Makamu wa Rais wa sasa, Dkt Philip Mpango, kutogombea tena.
Uteuzi wa Dkt Nchimbi umepokewa vema wilayani Songea na katika mkoa mzima wa Ruvuma ambako ndio anakotokea.
Mmoja kati ya walioonesha furaha yao ni Mwenyekiti wa Vijana wa CCM (UVCCM) wa Wilaya ya Songea, Joachim Komba, ambaye alisema Emmanuel Nchimbi kuwa watu wa mkoa huo wana furaha kubwa kuletewa Dkt Nchimbi kama mgombea mwenza.
“Wana Ruvuma na wana Songea tuna furaha kubwa ambayo haina mfano kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum kutuletea Dkt Emmanuel J. Nchimbi kuwa mgombea nafasi ya umakamu urais. Tunasema asante sana, sana, sana na sisi kama vijana wa CCM Songea Mjini tutawalinda viongozi wetu, tutawapigania viongozi wetu na tutahakikisha katika uchaguzi huu tunaenda kushinda ushindi wa kimbunga.”
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CCM Songea Mjini, Mwinyi Msolomi, amewataka vijana kuwaheshimisha wagombea urais walioteuliwa na kuonya dhidi ya tabia ya kuwachafua.
“Jukumu letu sisi ni kuwaheshimisha wagombea wetu. Tusianze kuwatia madoa, tunaelewana? Hakuna binadamu aliyekamilika. Tukianza kuwatia madoa, maana yake tunampa adui nafasi. Wenzetu tumesikia mkutano wao mkuu, wametiana madoa, sasa siku ya kumnadi unamnadi nani? Sisi tabia ile tusiilete, ile ni tabia ya watu ambao hawajakomaa kisiasa,” Msolomi alisema.
Written by Angel Kayombo, Ruvuma