Habari

Vijana waaswa kuchangamkia fursa za biashara ya asali

 

Vijana wanaaswa kuchangamkia fursa ya uzalishaji wa asali ili waweze kujipatia kipato na kujikwamua kimaisha, na watapewa mafunzo pamoja na mtaji wa kuanzisha biashara hiyo.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Ruvuma Kelvin Charles, wakati alipotembelea Kata ya Maguu Wilaya ya Mbinga Vijijini Mkoani Ruvuma. Ambapo alimtolea kama mfano aliyekuwa Waziri Mkuu, kwa jinsi gani zao hilo limemnufaisha.

“Asali ni biashara moja kubwa sana, waziri Mkuu Mstaafu mh.Pinda na mjumbe wetu wa kamati kuu amekuwa akiifanya kwa muda mrefu sana, na watu wengi ambao wanafanya mradi huo wengi ni matajiri”

“Tumeongea na ofisi ya Mkoa kupitia RASI, tupo kwenye mchakato, Kila wilaya itatoa vijana kumi, ambao wataenda wenye mafunzo, wakitoka kwenye mafunzo watapewa mtaji wa kuweza kutengeneza mizinga na kwenda kuvuna asali.”

Charles amesema kuwa, wao kama viongozi waliopewa dhamana na wananchi wanapaswa kuwapigania kwa kuwa ni wajibu wao.

“Sisi tutaendelea kuwatafutia fursa ndugu zangu, na ni wajibu wetu, mlivyotupa hizi dhamana tuliwaahidi tutaenda kuwapigania, na Mimi nipo tayari kuwapigania katika Kila namna.”

Vilevile Charles amewaasa vijana kuendelea kujitolea na kukipigania chama ili mwisho wa siku waweze kujipatia fursa mbalimbali

“Tuna Kila sababu ya kuwaunga mkono viongozi hawa na tuendelee kuwaheshimisha kwa mambo mazuri ambayo tunakiwa kuyafanya, lakini pia niwaombe vijana wenzangu, tuendelee kujitolea na kukipigania chama Cha mapinduzi mwisho wa siku tutapata fursa kupitia chama hiki.”

Aidha katika ziara hiyo aliyoifanya katika Kata hiyo ya Maguu, Charles amepongeza mradi wa kituo cha TRC Maguu, chenye madarasa mawili ya kujifunzia walimu, ambacho kimejengwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pamoja na wananchi wa kata hiyo kwa kujitolea katika shughuli mbalimbali.

“Nimepata fursa ya kuja kutembelea mradi huu, tumeuona, tumesomewa taarifa hapa Kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan alileta fedha hapa milioni 22, kwaajili ya ujenzi wa hili jengo, lakini pia tumeambiwa asilimia 20 ni nguvu kazi zetu ninyi wananchi, Mwenyezi Mungu awabariki sana kwa kazi hiyo kubwa mliyoifanya.”

Pia amewaomba sana wananchi hao kuusimamia na kuutunza mradi huo pamoja na thamani zitakaowekwa ili ziweze kutumika ipasavyo.

Written by Angel Kayombo, Ruvuma

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents