Vijana wahimizwa kushiriki shindano la ‘Vijana Uchumi Challenge’

Serikali imewahimiza vijana kote nchini kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika shindano jipya la kitaifa la “Vijana Uchumi Challenge,” likilenga kuimarisha ushiriki wao katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema shindano hilo ni fursa adhimu kwa vijana kuonyesha ubunifu wao na kuchangia maendeleo ya kiuchumi nchini.
Amesisitiza kuwa mpango huo haujalenga ushindani pekee, bali ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwapa vijana jukwaa la kuwasilisha mawazo ya kibunifu yatakayosaidia kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
“Halilengi tu kupata mawazo bunifu, bali pia kutoa fursa kwa vijana kuonyesha uwezo wao wa kutoa fikra chanya kwa ajili ya nchi yetu,” alisema Waziri Nanauka.
Waziri Nanauka alibainisha kuwa uzinduzi wa shindano hilo ni hatua ya makusudi ya kuhakikisha vijana wanashiriki moja kwa moja katika ujenzi wa uchumi wa taifa kupitia miradi na mawazo yao ya kibiashara.
Aidha, alieleza kuwa uongozi wa Samia Suluhu Hassan umeendelea kuweka mazingira rafiki kwa vijana, ikiwemo kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana chini ya Ofisi ya Rais ili kuongeza uratibu na uzito wa masuala ya vijana katika ngazi ya juu ya Serikali.
Katika hatua nyingine, Amina Sanga ameteuliwa rasmi kuwa Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya “Vijana Uchumi Challenge,” uteuzi uliofanywa kupitia Waziri Nanauka. Kupitia nafasi hiyo, anajiunga na timu inayosimamia utekelezaji wa jukwaa hilo muhimu la kitaifa.
Amina Sanga ana uzoefu wa zaidi ya muongo mmoja katika maendeleo ya vijana, ambapo ameweza kujijengea sifa ya kuwa miongoni mwa viongozi vijana wanaochangia katika kukuza vipaji na uwezo wa vijana nchini. Uzoefu wake unatarajiwa kusaidia katika kuhakikisha mafanikio ya utekelezaji wa mpango huo.
Kwa ujumla, uzinduzi wa shindano hilo pamoja na uteuzi wa viongozi wake unaashiria dhamira ya Serikali ya kuwajengea vijana mazingira bora ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Kupitia “Vijana Uchumi Challenge,” vijana wanatarajiwa kupata fursa ya kugeuza mawazo yao kuwa miradi halisi yenye tija, hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa na maendeleo ya kijamii.
Written by Janeth Jovin






