Habari

Waandishi wapigwa msasa namna ya kuripoti habari za uchumi

Katika jitihada za kuendeleza sekta ya habari nchini, Benki ya CRDB imeendesha semina maalum kwa waandishi wa habari za biashara na uchumi iliyofanyika katika Makao Makuu ya benki hiyo yaliyopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Akifungua semina hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa amesema semina hiyo iliyopewa jina la “CRDB Bank Media Day” imelenga kuwajengea uwezo na ujuzi waandishi wa habari ili kuweza kutekeleza majukumu yao ya kuihabarisha jamii kwa ufanisi na waledi mkubwa.

“Tukiwa wadau wakubwa wa sekta yaa habari tunajukumu la kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi yao vizuri kwa kuwaongezea maarifa yatakayowasidia kuandaa na kuhariri habari za biashara na uchumi kwa weledi mkubwa,” alisema Mwambapa.

Mwambapa alisema Benki hiyo imeona kuna pengo linaloongezeka la ubora wa habari za biashara na fedha kwenye vyombo vya habari msukumo uliopelekea kuandaa semina hiyo. Aliongezea kuwa mpango ni kuendelea kuandaa semina hiyo mara kwa mara ili kuinua kiwango cha taarifa za fedha.

Mkurugenzi huyo alisema mafanikio ya Benki ya CRDB yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na taarifa za vyombo vya habari kwa umma ambazo zilikuwa na matokeo chanya kwa jamii. “Vyombo vya habari sio tu vimesaidia kutangaza huduma na malengo ya Benki ya CRDB lakini pia utendaji wa uchumi wa taifa katika hatua mbalimbali,” alisema.

Alisema licha ya sera nzuri za uchumi za nchi kama vyombo vya habari vitapuuzwa malengo ya kuwawezesha watu kufahamu kinachoendelea katika mazingira yao na fursa zilizopo hayataweza kufikiwa.

Kutokana na umuhimu wa vyombo vya habari kuinua sekta mbalimbali za uchumi benki hiyo sasa imepania kuendelea kufadhili waandishi wa habari hususan katika tafiti zinazohusu masuala ya uchumi, fedha na taarifa za biashara ili kuwafikia wananchi wengi.

Akichangia mjadala wa “Jukumu la Vyombo la Habari katika Kukuza Uchumi” Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications, Bakari Machumu, alipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa semina hiyo kwa waandishi wa habari. Machumu alisema waandishi wa habari wanapaswa pia kujenga uelewa wa kutosha wa sekta mbalimbali jambo litakalowasidia katika kujenga hoja katika taarifa zao.

“Kujenga uelewa juu ya sekta husika kutamwezesha mtu sio tu kuandika taarifa bora bali pia kujenga uwezo wa kuhoji kutakakowezesha kupata taarifa zaidi,” Bw Machumu, ambaye pia ni mtaalamu wa habari za biashara, alisema wakati wa kongamano hilo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents