Habari

Wafanyakazi KRA kuvaa kamera katika kukusanya kodi

Mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini Kenya, KRA imetangaza kuwa wafanyakazi wake wataanza kutumia kamera za mwili ili kudhibiti udanganyifu wa ushuru, upokeaji wa rushwa na wafanyakazi wake na pia kuzuia kukwepa kufanya malipo mengine ya ushuru.

Mamlaka hiyo imevieleza vyombo vya habari vya Kenya kuwa kamera hizo zitakazonasa video zitatumiwa hasa na wafanyakazi wake katika idara ya ushuru ya ndani na forodha na maeneo ya udhibiti wa mipaka, anavyotuarifu Mwandishi wetu wa Nairobi, Kennedy Wandera.

Katika mahojiano ya kipekee na gazeti la Business Daily nchini Kenya, James Githii Mburu ambaye ni Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, ameeleza kuwa hatua ya kuanzishwa matumizi ya kamera hizo kwa wafanyakazi wake ni mkakati thabiti wa kupambana na ufisadi unaojidhihirisha kupitia ukwepaji wa ulipaji ushuru, upokeaji wa rushwa na wafanyikazi wake na pia kuzuia kukwepa kufanya malipo mengine ya ushuru yanayostahiki.

Gazeti hilo linamnukuu afisa huyo wa ngazi ya juu katika mamlaka hiyo akieleza kuwa wafanyakazi wake katika idara ya kodi ya ndani na forodha na udhibiti wa mpaka, watavaa kamera hizo zilizo na uwezo mkubwa wa kunasa na kuhifadhi video za matukio kipindi chote afisa wake anapokuwa kazini.

Wapi kamera zitatumika?

Matumizi ya kamera yataanza katika mipaka ya Kenya, bandari ya Mombasa, Mabohari ya makontena na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) ambapo vitendo vya uhalifu vinavyohusiana na ukwepaji kodi, wizi, ufisadi, utapeli, kuingizwa kwa mizigo ambayo haijatangazwa na bidhaa nyingine za magendo, rushwa na visa vya utakatishaji fedha vimeripotiwa.

Madai ya uingizaji mizigo kwa njia ya udanganyifu na ubadilishaji wa fomu za ushuru ili kusaidia watu kukwepa malipo ya ushuru yameelekezewa baadhi ya maafisa wa mamlaka hiyo, gazeti hilo limeripoti.

“Hivi karibuni pia tutahakikisha maafisa wetu wa utekelezaji wana kamera zinazovaliwa kama hizi unazoziona huko Marekani, ili hatua yoyote watakayochukua irekodiwe na sisi tuione. Ukiizima, tutakuwa tunahitaji kuelewa ni kwa nini unafanya hivyo,” Kamishna Mkuu wa KRA Githii Mburu ameliambia gazeti la Business Daily, ambalo pia linaeleza kuwa mamlaka hiyo hupoteza zaidi ya shilingi bilioni 12 kila mwaka kutokana na ukwepaji wa ushuru.

Wataalam wanasemaje?

Alvin Mosioma, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Tax Justice Network Africa, mtaalam wa uhamiaji na mifumo ya kodi anaeleza kuwa njia hiyo ni bunifu lakini haisuluhishi matatizo yote.

Mosioma vile vile anaeleza kuwa KRA inastahili kuongeza matumizi mengine ya mifumo ya kiteknolojia na vile vile kuboresha mishahara ya wafanyakazi wake kuondoa mazoea ya uhalifu.

Na ili kupambana na ukwepaji wa ushuru unaoendelezwa na watengenezaji wa vileo, KRA pia, inalenga kuboresha ufuatiliaji katika majengo yanayozalisha bidhaa hizo zinazotozwa ushuru kupitia video halisi ya CCTV ili kufuatilia mienendo ya bidhaa hizo.

Katika bejeti yake ya 2022/23 yenye maudhui ya “Kuongeza kasi ya kufufua uchumi ili kuboresha na kunawiri mapato”, serikali ya Kenya, inatarajia kupata makusanyo ya ushuru wa shilingi trilioni 2.4 ambao ni asilimia 17% ya pato la taifa kuziba mapungufu ya bejeti yake ya shilingi trillioni 3.3 lakini mamlaka hiyo ya ushuru inapania kufunga mianya ya ukwepaji ushuru ili kufikia malengo yake ya kuongeza mapato ya serikali.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents