Habari

Wafanyakazi tisa wa kujitolea kutoka Japani wawasili Tanzania kusaidia miradi ya maendeleo

Wafanyakazi wapya tisa wa kujitolea kutoka Japan waliwasili Tanzania ikiwa ni sehemu ya mpango unaoendelea wa kuunga mkono juhudi za maendeleo ya nchi katika sekta mbalimbali.

Wajapani hao wa kujitolea watakuwa katika maeneo yafuatayo, watatu Dodoma, wawili Moshi, watatu Morogoro na mmoja Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) imeeleza kuwa kuwasili kwao kunafanya jumla ya wafanyakazi wa kujitolea waliotumwa Tanzania tangu janga la COVID-19 kufikia 28, huku 19 wakiwa tayari wametumwa kabla ya kundi hilo.

Imeeleza kuwa mpango huo umewafanya wajitoleaji waliowasili Tanzania tangu kuanzishwa kwake kufikia 1,717 na kwamba mpango hu oni muhimu katika kukuza ushirikiano na maendeleo ya kimataifa.

“Kuwasili kwa wafanyakazi hao wa kujitolea kunaonyesha ushirikiano imara na wa kudumu kati ya Tanzania na JICA unaosisitiza kujitolea kwa pamoja katika kuboresha maisha na kujenga uwezo katika kanda. Mpango huu wa kujitolea ujulikanao Japan Overseas Cooperation Volunteers (JOCV) uliozinduliwa na JICA mnamo Desemba 1965, umetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kimataifa.

“Tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umetuma watu wa kujitolea 57,172 kwa nchi 130. Kufikia Julai 31, 2024, kuna wafanyakazi wa kujitolea 1,394 wanaofanya kazi katika nchi 78. Mpango wa JOCV huajiri watu binafsi walio na ujuzi na uzoefu unaofaa ili kukidhi mahitaji mahususi ya nchi zinazoendelea,” imeeleza taarifa hiyo

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa nchini Tanzania, ambapo programu ya JOCV ilianza Machi 1967 ikiwa na timu ya watu 30 wa kujitolea, mwelekeo umebadilika kwa miaka mingi.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents