Wagonjwa wapya wa saratani 42,000 hugundulika kila mwaka nchini

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Faraja Kiwanga, amesema kuwa takribani wagonjwa wapya wa saratani 42,000 hugundulika kila mwaka nchini, huku watu zaidi ya 28,000 hupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Dk. Kiwanga ametoa takwimu hizo leo jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo ya siku moja yaliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), yenye lengo la kuongeza uelewa kwa wanahabari wanawake na jamii kuhusu uchunguzi wa mapema na kinga dhidi ya saratani ya matiti.
Amesema idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na saratani inachangiwa na ukweli kwamba wagonjwa wengi hufika hospitalini wakiwa katika hatua za tatu au nne za ugonjwa huo, jambo linalowapa changamoto madaktari katika kutoa tiba kamili.
“Bado tunakazi kubwa ya kuendelea kutoa elimu kwa umma ili watu wafanye uchunguzi mapema. Takribani asilimia 75 ya wagonjwa wanaofika hospitalini, hufika wakiwa katika hatua za mwisho za saratani. Kufanya uchunguzi mara kwa mara kunasaidia kugundua ugonjwa katika hatua za awali ambazo tiba yake ni rahisi na mtu anaweza kuishi kwa muda mrefu,” amesema Dk. Kiwanga.
Amefafanua kuwa saratani inayoongoza kwa wanawake ni saratani ya mlango wa kizazi, ikifuatiwa na saratani ya matiti, utumbo mkubwa na mdogo, koo, kichwa na shingo. Kwa upande wa wanaume, saratani inayoongoza ni ya tezi dume, ikifuatiwa na koo la chakula, utumbo mkubwa na mdogo, pamoja na matezi.
Kuhusu visababishi vya saratani, Dk. Kiwanga ametaja miongoni mwao kuwa ni ulaji wa vyakula vilivyoharibika au vilivyokaa muda mrefu, ulaji wa nyama nyekundu kupita kiasi, unene uliopitiliza, matumizi ya tumbaku na pombe kwa muda mrefu, kutofanya mazoezi, pamoja na matumizi ya kemikali na mionzi hatarishi.
Amesisitiza kuwa kadri umri wa mtu unavyoongezeka, ndivyo hatari ya kupata saratani inavyokuwa kubwa zaidi, huku baadhi ya watu wakipata ugonjwa huo kwa sababu ya kurithi katika familia.
Aidha, ameeleza kuwa takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa kila mwaka wagonjwa wapya wa saratani duniani hufikia takribani milioni 18, huku watu zaidi ya milioni 9 wakifariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
“Kwa mujibu wa takwimu hizo, zaidi ya watu milioni 43 duniani wanaishi na saratani. Hii inaonyesha kuwa saratani ikigundulika mapema, tiba inapatikana na wagonjwa wanaweza kuendelea kuishi maisha ya kawaida,” amesema Dk. Kiwanga.
Written by Janeth Jovin







